Michezo

Bale afungua upya akaunti yake ya mabao kambini mwa Spurs

November 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

GARETH Bale alifungua upya akaunti yake ya mabao kambini mwa Tottenham Hotspur mnamo Jumapili na kusaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Brighton.

Ushindi huo uliwakweza Spurs hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 14, mbili nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi, Liverpool.

Fowadi na nahodha Harry Kane aliwaweka Spurs kifua mbele kunako dakika ya 13 kupitia penalti kabla ya Lamptey kusawazisha kupitia Tariq Lamptey katika dakika ya 56. Bao lilifumwa wavuni na Kane lilikuwa lake la 149 hadi kufikia sasa kwenye soka ya EPL.

Goli la Bale lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na sajili mpya Sergio Reguilon katika dakika ya 73. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa fowadi huyo aliyetokea Real Madrid kwa mkopo mwishoni mwa msimu uliopita kufungia Spurs tangu Mei 2013.

Bale alisherehekea bao hilo kwa mbwembwe nyingi, tukio ambalo kocha Jose Mourinho alifafanua kuwa ishara ya mambo makuu zaidi kutarajiwa kutoka kwa sogora huyo aliyekosekana kwenye mipango ya baadaye ya Real na mkufunzi Zinedine Zidane.

Brighton walisakata mchuano huo bila ya huduma za wavamizi wao matata, akiwemo Neal Maupay. Mechi hiyo ilimpa kocha Graham Potter wa Brighton fursa ya kumwajibisha kipa Robert Sanchez kwa mara ya kwanza.

“Tunahitaji mabao na nimekuwa nikisema kwamba Bale atahitaji wingi chache sana kambini mwa Spurs kabla ya kuanza kufunga magoli muhimu. Japo sidhani amerejea kabisa katika hali ya kuwajibishwa kwa jumla ya dakika 90 katika mechi moja, anazidi kuimarika na tunatarajia makuu kutoka kwake,” akasema Mourinho.

Bale alisajiliwa na Spurs kwa mara ya kwanza mnamo 2007 kwa kima cha Sh700 milioni. Mbali na kunyanyua mataji manne ya UEFA akiwa Real, pia alisaidia miamba hao wa soka ya Uhispania kutwaa makombe mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na mataji matatu ya Kombe la Dunia.

Bale anasalia kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza na ndiye Mwingereza (Wales) anayejivunia kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya Uhispania. Aliwafungia Real jumla ya mabao 80 na kuchangia mengine 40 katika jumla ya mechi 171.

Kiini cha kubanduka kwake Real ni kudorora kwa uhusiano kati yake na kocha raia wa Ufaransa, Zidane.

Kwa kumsajili Bale kwa Sh11 bilioni, Real walivunja rekodi ya Sh10.8 bilioni walizoweka mezani mnamo 2009 kwa minajili ya huduma za nyota raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo mnamo 2009.

Katika mkataba wake wa kwanza wa miaka sita, Bale alikuwa akilipwa na Real mshahara wa Sh42 milioni kwa wiki kabla ya kutia saini mkataba mwingine wa miaka sita mnamo 2016 ambapo alikuwa akilipwa Sh84 milioni kwa wiki.

Spurs kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Ludogorets ya Bulgaria katika mechi ijayo ya Europa League mnamo Novemba 5 huku Brighton wakitarajiwa kuwaalika Burnley ugani Amex kwa minajili ya gozi la EPL mnamo Novemba 6, 2020.