Michezo

Bale aisaidia Madrid sare dhidi ya Villarreal

September 3rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Gareth Bale aliwafungia Real Madrid mabao mawili kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyowakutanisha na Villarreal wikendi iliyopita.

Bale ambaye alikuwa tayari kubanduka uwanjani Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu jana, alilishwa kadi mbili za manjano katika mchuano huo uliomshuhudia akifuta ukame wa siku 169 bila ya kufunga bao katika kivumbi cha La Liga.

Awali, Villarreal walikuwa wamejipa uongozi wa mapema kupitia kwa Gerard Moreno kabla ya Bale kufungua akaunti ya mabao yake mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Moi Gomez aliwarejesha Villarreal mchezoni kabla ya Bale kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mabao ya Bale yalikuwa ya kwanza tangu kocha Zinedine Zidane asisitize kwamba kuondoka kwa nyota huyo kambini mwa Real kungeleta afueni tele uwanjani Bernabeu.

Real walitamalaki mchezo katika kipindi cha pili huku fowadi Toni Kroos akimfanyiza kipa Andres Fernandez kazi nyingi ya ziada. Bao la Karim Benzema ambalo lingewavunia Real ushindi lilifutiliwa mbali na refa kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Bale ambaye ni mzawa wa Wales anakuwa mchezaji wa pili wa Real baada ya Cristiano Ronaldo kupachika wavuni mabao mawili katika mechi moja ya La Liga kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi iyo hiyo.

Matokeo hayo yaliwakweza Real hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama tano sawa na Alaves na Osasuna ambao limbukeni wa kipute hicho.

Villarreal kwa upande wao wanashikilia nafasi ya 16 kwa alama mbili sawa na Getafe walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya Alaves.

Bale ambaye amewahi kuwachezea Tottenham Hotspur kabla ya kurasimisha uhamisho wake hadi Uhispania kwa kima cha Sh11 bilioni mnamo 2013, angali na miaka mitatu katika mkataba wake na Real.

Fowadi huyu mwenye umri wa miaka 30 alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning ya China msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki. Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, maamuzi ya Real kuzuia uhamisho wa Bale katika dakika za mwisho yalichochewa na mambo mawili. Mosi, walitaka Suning walipie ada yote ya kumsajili pili, ni jeraha litakalomweka winga Marco Asensio mkekani kwa kipindi kirefu katika msimu wa 2019-20.