Michezo

'Bale haondoki Madrid'

July 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

GARETH Bale anafurahia maisha yake kambini mwa Real Madrid na haendi popote licha kwamba amekiri “kuhangaishwa” na kocha Zinedine Zidane.

Bale ambaye ni mzawa wa Wales, alidhihirisha wazi kukerwa kwake na hatua ya kuachwa na Zidane nje ya kikosi alichokitegemea katika mchuano wa mwisho wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu dhidi ya Leganes. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya 1-1.

Japo vikosi vingine vimefichua maazimio ya kumsajili Bale, Jonathan Barnett ambaye ni wakala wa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 31 amesema mteja wake hatabanduka kambini mwa Real na kujiunga na kikosi kingine ama kwa mkataba wa kudumu au kwa mkopo.

“Bale angali na miaka miwili zaidi katika mkataba wake wa sasa na Real. Anafurahia maisha yake na ya familia yake jijini Madrid na hataondoka kwenda popote. Anaridhika kila anapovalia jezi za Real. Kibarua kwa sasa kipo kwa Zidane, si kwa Bale,” akatanguliza Barnett.

“Ingawa zipo klabu zinazomhemea, sioni kikosi chochote kati ya hivyo vinavyowania maarifa yake kinachoweza kumudu bei yake. Ni pigo kubwa sana kwamba kwa sasa hajakuwa akiunga kikosi cha kwanza cha Real. Licha ya kuhangaishwa huko, hatahiari kuondoka,” akasema Barnett.

Kufikia sasa, Bale anajivunia kufungia Real zaidi ya mabao 100 na kushindia miamba hao wa soka ya Uhispania mataji manne ya La Liga. Hata hivyo, tetesi kuhusu kuagana kwake na Real zimekuwa nyingi hasa ikizingatiwa uhusiano mbaya kati yake na Zidane.

Miongoni mwa sababu zilizochangia kuondoka kwa Zidane kambini mwa Real mnamo 2018 ni kukosana kwake na Rais Florentino Perez kuhusiana na Bale. Huku Perez akimtaka Bale kusalia uwanjani Santiago Bernabeu, Zidane alitaka sana aondoke.

Bale kwa sasa ndiye mchezaji anayedumishwa kwa mshahara mkubwa zaidi kambini mwa Real. Nyota huyo hutia kapuni kima cha Sh84 milioni kwa wiki. Hiyo ndiyo sababu kubwa ambayo inawasukuma Real kutaka kumtia mnadani ili kupunguza gharama ya matumizi.

Bale alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning ya China kwa mkataba wa miaka mitatu mwanzoni mwa msimu huu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Hata hivyo, Real walizuia uhamisho wake katika dakika za mwisho kwa sababu walitaka Suning walipie ada yote ya kumsajili na pia walikuwa bado wakimhitaji baada ya winga Marco Asensio kupata jeraha.

Inter Miami ya kocha David Beckham nchini Amerika iko tayari kuweka mezani Sh7 bilioni kwa minajili ya huduma za Bale ambaye anawaniwa pia na Newcastle United na Tottenham Hotspur.

Bale aliondoka Tottenham mnamo Septemba 2013 kwa kima cha Sh11 bilioni na amewashindia Real mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Kombe la Dunia miongoni mwa klabu, matatu ya Uefa Super Cup na moja la Spanish Super Cup.