Michezo

Bale hawezi kurudi EPL – Ajenti

June 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA Gareth Bale hataki kurejea tena kusakata soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na dalili zote zinaashiria kwamba ataangika daluga zake ulingoni akivalia jezi za Real Madrid. Haya ni kwa mujibu wa wakala wake, Jonathan Barnett.

Bale, 30, amekuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea Tottenham Hotspur au kuingia katika sajili rasmi ya Newcastle United mwishoni mwa msimu huu baada ya uhusiano wake na kocha Zinedine Zidane kuvurugika uwanjani Santiago Bernabeu.

Fowadi huyo mzawa wa Wales aliondoka Tottenham mnamo Septemba 2013 kwa kima cha Sh11 bilioni na amewashindia Real mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), moja la La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Kombe la Dunia miongoni mwa klabu, matatu ya Uefa Super Cup na moja la Spanish Super Cup.

Bale mwenye umri wa miaka 30 alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning ya China mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Hata hivyo, Real walizuia uhamisho wake katika dakika za mwisho kwa sababu walitaka Suning walipie ada yote ya kumsajili na pia walikuwa bado wakimhitaji baada ya winga Marco Asensio kupata jeraha.

Inter Miami ya kocha David Beckham nchini Amerika pia iko tayari kuweka mezani Sh7 bilioni kwa minajili ya huduma za Bale.

“Anafurahia maisha yake jijini Madrid. Sioni sababu itakayomfanya kutostaafu akiwa mchezaji wa Real,” akatanguliza Barnett.

“Iwapo ni pesa, anazo. Aidha, ameshinda takriban mataji yote ya haiba kubwa katika ulingo wa soka isipokuwa Kombe la Dunia miongoni mwa mataifa. Bahati mbaya yeye ni mchezaji wa Wales na doto ya kuongoza taifa hilo kutwaa ubingwa wa dunia huenda isitimie,” akasema Barnett.

Kupungua kwa mapato ya Real msimu huu kutokana na janga la corona kunatarajiwa pia kuwaweka miamba hao wa soka ya Uhispania katika ulazima wa kuwatia baadhi ya wanasoka wao mnadani mwishoni mwa muhula huu.

Miongoni mwao ni kiungo mvamizi wa Colombia, James Rodriguez aliyewahi pia kuchezea Bayern Munich kwa mkopo.