Michezo

Bale katika hali tete ndani ya Real Madrid

May 21st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

RAIS wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon amesema kwamba “itakuwa vigumu” kwa nyota Gareth Bale kusalia uwanjani Bernabeu baada ya kampeni za muhula huu kutamatika.

Bale alisalia benchi mwishoni mwa wiki jana waajiri wake Real Madrid waliposajili matokeo duni kwa kupepetwa 2-0 na Real Betis mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ugani Santiago Bernabeu.

Kulingana na Calderon, ambacho Bale alitarajiwa kufanya mwishoni mwa mchuano wao na Betis ni kuwaaga rasmi mashabiki wa Real, jambo ambalo hakufanya.

“Pengine angali na tumaini la kusalia ugani Santiago msimu ujao. Sidhani hilo litawezekana. Alistahili kuaga mashabiki mwishoni mwa mechi dhidi ya Betis,” akasema.

Calderon anaamini kwamba muda wa kuhudumu kwa Bale kambini mwa Real utatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu baada ya kipindi cha miaka sita tangu aliposajiliwa kwa kima cha Sh11 bilioni kutoka Tottenham Hotspur.

Bale, 29, anatarajiwa kusajiliwa na Manchester United au kurejea kambini mwa Tottenham japo huenda hatua hiyo ikamchochea Harry Kane kubanduka na kuyoyomea Real iwapo waajiri wake wa sasa watashindwa kusawazisha mshahara wake na malipo ambaye Bale atakuwa akipokezwa.

Kwa upande wake, kocha Zinedine Zidane wa Real amesema kwamba mustakabali wa Bale ambaye ni mzawa wa Wales, utaamuliwa mwishoni mwa msimu huu.

Licha ya kuwasaidia Real kutia kapuni jumla ya mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Bale bado amekosa kuwa kipenzi cha mashabiki wengi ugani Bernabeu, Uhispania.

Japo majeraha yamekuwa kiini cha kusuasua kwa Bale katika ngazi za klabu na timu ya taifa, Zidane anahisi kwamba nyota huyo angali na ushawishi mkubwa katika kikosi cha Real licha ya madai kwamba hahusiani vyema na masogora wenzake.

Manchester United

Man-United wamekuwa wakihusishwa na Bale tangu 2013 alipobanduka Tottenham Hotspur nchini Uingereza na kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Real.

Man-United wako radhi kuweka mezani kima cha Sh7 bilioni ili kumsajili Bale.

Iwapo wataambulia pakavu katika juhudi zao za kusajili Bale, Man-United watapania kumhemea zaidi Philippe Coutinho wa Barcelona.

Hata hivyo, kutua kwa Bale ugani Old Trafford ni biashara itakayokuwa zao la makubaliano kwamba Paul Pogba wa Man-United anayoyomea Uhispania kuwawajibikia Real ambao pia wanazihemea huduma za Eden Hazard, Kylian Mbappe na Christian Eriksen wa Chelsea, PSG na Tottenham mtawalia.