Michezo

Bale kujiondoa Madrid akipata mwanya

October 9th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

MSHAMBULIAJI matata Gareth Bale wa Real Madrid ameeleza kukasirishwa na kuchoshwa kwake kama sababu ya kutaka aagane na klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Uhispania, La Liga.

Bale alitarajiwa kujiunga na klabu ya Jiangsu Suning inayoshiriki ligi kuu ya China kwa mkataba wa miaka mitatu wakati wa msimu wa uhamisho uliopita. Alitarajiwa kulipwa Sh127 milioni kwa wiki- lakini Real Madrid wakamzuia wakisisitiza hawezi kuondoka kama mchezaji huru.

Mnamo Julai, kocha Zinedine Zidane wa Madrid alinukuliwa akisema “ni vyema aondoke mapema”, tamko ambalo ajenti wa mchezaji huyo, Jonathan Barnett alisema lilikuwa la kidharau kwa mchezaji ambaye alikuwa ameifanyia timu hiyo makubwa.

Bale ameisaidia Madrid kutwaa mataji manne ya Klabu Bingwa barani Ulaya, moja la La Liga, moja la Copa del Rey na matatu ya Uefa Super Cups pamoja na mengine ya Club World Cups, mbali na kuifungia klabu hiyo zaidi ya mabao 100.

Baada ya mpango wake wa kuhamia China kutibuka, nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alijiondoa kwenye kikosi kilichokuwa kikijiandaa kupimana nguvu na Bayern Munich kwa ajili ya msimu mpya, huku kukiwa na madai kwamba matamshi ya kocha wake hayakumfurahisha.

Alirejea na kufikia sasa tayari ameifungia Madrid mabao mawili katika mechi saba na sasa timu hiyo inaongoza msimamo wa La Liga.

Club Brugge

Lakini aliachwa nje ya kikosi kilichocheza na Club Brugge na kuagana kwa 2-2 na pia hakuwa kwenye kikosi kilichocheza na kushinda Granada 4-2, mwishoni mwa wiki.

Vyombo vya habari vimedai kwamba nyota huyo ameanza kupuuzwa baada ya kurejea katika kiwango chake bora.

“Amekasirika, amechanganyikiwa. Mara tu aliporejea klabuni, Zidane aliamua kumpuuza kabisa Bale, bila kueleza sababu kamili ya uamuzi wake.

“Bale tayari aliambiwa hayumo katika mipango ya Zidane ya msimu huu, na itabidi aondoke ili apate timu mpya ya kuchezea.

Ajenti wake, Jonathan Barnett, alianzisha mipango ya kumtafutia timu mpya, lakini Bale akaamua abakie klabuni msimu huu.

“Kinachomuudhi zaidi ni, kwa nini mipango ya kuondoka ilifunguliwa, lakini baadaye wakamzuia kuondoka. Madrid ilikataa kumuachilia ajiunge na Jiangsu Suning, baada ya madai kwamba klabu nyingine ya China ilikuwa ikijiandaa kutoa hela nyingi, habari ambazo ziliibukia kuwa za uwongo.

Kwa sasa, imesemekana Bale anapendelea zaidi kucheza gofu kuliko soka, na yuko tayari kabisa kuondoka iwapo atapata pa kwenda.

Amekuwa akiingia uwanjani kwa dakika chache na kucheza vizuri zaidi na hata kufunga mabao, kitu ambacho timu hiyo haifanyi bila yeye.