Michezo

Bale na Ramsey warejea katika kikosi cha Wales kwa mechi tatu zijazo dhidi ya USA, Jamhuri ya Ireland na Finland

November 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

GARETH Bale amerejea katika timu ya taifa ya Wales kwa minajili ya mechi tatu zijazo zitakazosimamiwa na kocha msaidizi wa kikosi hicho, Robert Page.

Page atasimamia michuano hiyo baada ya kocha mkuu Ryan Giggs kukabiliwa na shutuma za kumjeruhi mchumba wake.

Tukio hilo lilimfanya kutiwa nguvuni na maafisa wa polisi jijini Cardiff kwa uchunguzi zaidi.

Bale ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Wales hakuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki mechi za kimataifa za mwezi Oktoba 2020. Wakati huo, Bale alikuwa akijifanyia mazoezi kwa minajili ya kuanza kampeni za Tottenham Hotspur baada ya kujiunga upya na kikosi hicho kwa mkopo kutoka Real Madrid.

Bale, 31, alipata jeraha la goti mnamo Septemba 2020 wakati akichezea Wales dhidi ya Bulgaria.

Mechi tatu zijazo zitakazomshuhudia Bale akichezea Wales ni dhidi ya Amerika, Jamhuri ya Ireland na Finland.

Mbali na Bale, nyota mwingine atakayetegemewa pakubwa na Page katika vibarua hivyo ni nyota wa zamani wa Arsenal, Aaron Ramsey ambaye kwa sasa anachezea Juventus.

Ramsey amejumuishwa katika kikosi hicho cha Wales licha ya kupata jeraha la misuli kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha Juventus na Ferencvaros. Juventus ya kocha Andrea Pirlo ilishinda mechi hiyo kwa 4-1 mnamo Novemba 4, 2020.

Baada ya kucheza na Amerika kirafiki mnamo Novemba 12, 2020 uwanjani Liberty, Wales watachuana na Jamhuri ya Ireland uwanjani Cardiff City mnamo Novemba 15 katika mojawapo ya mechi mbili za UEFA Nations League kabla ya kuchuana na Finland mnamo Novemba 18.

Wales wamewajumuisha katika kikosi chao makipa wapya baada ya Wayne Hennessey (Crystal Palace) na Adam Davies (Stoke City) kupata majeraha.

Kipa wa Dunfermline, Owain Fon Williams na Tom King wa Newport County wameitwa kambini kujaza nafasi za wawili hao wanaougua.

Newport ambao wanaongoza jedwali la Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uingereza (League Two) wana wachezaji wawili katika timu ya taifa ya Wales kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 37. Iwapo yeyote kati ya wawili hao atawajibishwa, basi itakuwa mara ya kwanza tangu Juni 1983 dhidi ya Brazil.

Sheehan ni mmoja kati ya wachezaji watatu kwenye orodha ya wanasoka 29 ambao wameitwa kambini mwa Wales. Wengine ni King na kiungo wa Nottingham Forest, Brennan Johnson.

Wales wamewaita pia kikosini mwao mabeki James Lawrence na Tom Lockyer pamoja na viungo Tom Lawrence. Hal Robson-Kanu anauguza jeraha la mkono huku Sam Vokes akikosa kabisa kuitwa kambini bila sababu.

Kwa upande wao, Amerika wamejumuisha kikosini nyota wa Chelsea, Christian Pulisic na kipa wa Manchester City, Zack Steffen katika timu itakayocheza dhidi ya Wales na Panama.

KIKOSI CHA WALES:

Ward, Fon Williams, King, Gunter, Davies, Roberts, Ampadu, Mepham, Lockyer, Rodon, N Williams, Lawrence, Cabango, Norrington-Davies, Ramsey, J Williams, Wilson, Brooks, James, Smith, Morrell, Levitt, Johnson, Sheehan, Bale, Lawrence, Moore, Ratondo, Roberts.