Makala

BALLET: Densi ya majuu inavyonoa akili za watoto Nakuru

July 17th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Densi ya Ballet yenye asili ya Uhispania na Uingereza inahitaji miondoko ya aina yake, utafiti ukionyesha kuwa watoto kati ya miaka 2-12 wataimarisha afya, upevu na ukomavu wa akili wakishiriki.

Densi yenyewe haiwezi kufananishwa na zile za kawaida kwa sababu mshiriki anahitajika kuwa makini, katika harakati za kuboresha stadi yenyewe hatua ya mwanzoni kabla hajahitimu na kuwa mahiri.

Taifa Leo Dijitali ilipatana na wanafunzi kadhaa wanaojifundisha Ballet kutoka mtaa wa Pipeline, Lanet viungani mwa mji wa Nakuru, siku ya Jumamosi baada ya masomo.

Bi Rosie Njoroge ,mwalimu wao alianzisha studio ndogo ya kunoa vipaji vya mabinti hawa wadogo akilenga kutumia fursa yenyewe kama hamasa ya kushinikiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

Bi Njoroge anaungama kuwa wanafunzi wanaoshiriki densi walikuwa ni mahiri sana darasani hasa ijapo katika somo la hisababi, miongoni mwa masomo mengineyo yanayotahiniwa shuleni.

“Wanatakiwa kujihami na stadi ya kuhesabu nambari za tarakimu, kwa sababu hii ndiyo njia ya kipekee itakayowafanya kukumbuka mafunzo yaliyotangulia,” Bi Rosie akasema.

Ingawa baadhi yao ni wadogo, wao huchukua muda mfupi sana kuiga na hatimaye wakabobea kwa kutegemea kasi ya mtoto kujifundisha.

Muziki tulivu ni kiungo muhimu kinachohitajika kunogesha shughuli hapa, ikizingatiwa kuwa kila hatua inategemea midundo inayoendana sawia na miondoko.

Kulingana na Bi Rosie, densi ya Ballet imekuwa ikiwasaidia wanafunzi kuongeza nguvu katika viungo vyao vya mwii, hasa wenye umri mdogo wanaoendelea kukua.

Humsaidia mwanafunzi kupata uzoefu na kufanya mambo ya kawaida kwa njia rahisi kama vile kucheza mpira na kushiriki michezo ya yoga inayohitaji viungo dhabiti vyenye unyumbufu.

Mbali na kufanya umbo la mshiriki kukomaa kwa haraka, Ballet humsaidia mwanafunzi kupata umbo linalopendeza.

Rosie anaona kuwa ipo haja kubwa kwa wanafunzi kuhimizwa kuhusu utumiaji wa vipaji vyao,kwa mujibu wa nyanja mbalimbali ili kujiendeleza kwenye nyanja mbalimbali za kimaisha.

Mshiriki anaweza kufanya vyema hata akahitimu na kufikia kiwango cha kimataifa kisha akajiajiri na kuwaajiri wengine katika ulingo unaokaribiana na huu ama huu.

“Ni njia mwafaka ya kupitiza muda miongoni mwa wanafunzi hasa wikendi ambapo wao huwa nje ya darasa,wanaweza kupata ujuzi wa maisha vilevile,” aliongezea.

Densi ya Ballet inalenga wanafunzi kutoka familia za tabaka la chini na wale wa tabaka la juu.

Hususan hii ikiwa ni densi ya kigeni inawahimiza watoto kujivunia tamaduni zao, na kuheshimu desturi za jamii nyinginezo zinazokaa pembe mbalimbali duniani.

Kinyume na zamani ambapo mchezo huu ulihusishwa kwa asilimia kubwa na wale wanaotokea katika tabaka la juu lakini kufikia sasa Ballet imepenya.

Maeneo mengine ambayo watoto wanashiriki densi hii ni kaunti ya Nairobi mtaa wa Kibera na Mombasa.

Rosie anawashauri wazazi kuwaruhusu watoto wao kujifunzi mambo mchanganyiko wangali wachanga,,kwa sababu hili litawasaidia kujitambua na kujielewa wakiwa na umri mdogo.

“Watoto kutoka kwenye familia maskini wanaamini kuwa hii ni mojawapo ya njia itakayowakwamua kutoka kwenye lindi la umaskini siku za usoni,” alisema.