Habari Mseto

Balozi azirai na kufariki ghafla akiwa benki

October 23rd, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

BALOZI wa Sudan Kusini nchini Eritrea Michael Nyang alizimia na kufariki ndani ya Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Moi Avenue, Kencom, Nairobi, Alhamisi.

Balozi huyo alikuwa ameenda kwenye benki hiyo kutoa pesa alipopatwa na matatizo ya kiafya kabla ya kuzimia na hatimaye akakata roho papo hapo.

Jitihada za madaktari walioitwa na wakuu katika benki hiyo kumsaidia hazikufua dafu kwa vile balozi huyo aliaga mwendo wa saa saba mchana. Balozi wa Sudan Kusini nchini Kenya Chol Ajongo alithibitisha kifo hicho lakini hakutoa maelezo zaidi hadi familia ya mwenda zake ijulishwe kwanza.

“Nathibitisha kwamba tumempoteza mmoja wetu. Aliaga jijini Nairobi alasiri. Sitatoa maelezo zaidi hadi tujulishe familia yake,” Bw Ajongo aliambia Taifa Leo.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nairobi Rashid Yakub pia alithibitisha kifo hicho ndani ya Benki ya KCB alipokuwa ameenda kutoa pesa katika kitengo cha watu mashuhuri (VIP).