Kimataifa

Balozi wa Amerika akwama kwenye lifti

February 21st, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

BALOZI wa Amerika nchini Kyle McCarter mnamo Alhamisi alionja hali halisi ya kuwa Kenya baada ya kukwama kwenye lifti kwa karibu nusu saa alipokuwa akielekea kutoa hotuba yake kuhusu afya nchini Kenya.

Mjumbe huyo alikuwa akisubiriwa kuzungumzia ripoti kuhusu Utathmini wa Madhara ya HIV kutokana na Idadi ya Watu (KENPHIA) katika jumba la Afya House, kabla ya kukumbana na masaibu hayo.

Bw Carter, anayefahamika kwa uchangamfu wake, alichagua badala yake kucheka masaibu yake kwa kujitosa mitandaoni huku akiambatisha picha yake pamoja na maafisa wengine wakiwa wamekwama ndani ya lifti.

“Amini usiamini nilikwama ndani ya lifti kabla ya kutoa hotuba kutangaza habari njema za ufanisi dhidi ya HIV nchini Kenya,”

Balozi huyo alifichua ilikuwa yake ya kwanza kujipata katika hali hiyo huku akisema alipata funzo muhimu la ‘kutumia vidato kila mara unapoenda katika hafla ya afya.’

“Haijawahi kunitendekea tena hapo awali lakini sasa nina kisa cha kusimulia. Funzo ni kwamba, kila wakati tumia vidato unapoenda katika hafla ya afya. Kauli hiyo inasikika kuwa na maana!”ulisema ujumbe wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Picha yake ilisambazwa mitandaoni huku Wakenya kama kawaida yao wakifurika kwenye ukurasa wake kwa jumbe za kuvunja mbavu wakimfahamisha matatizo hayo hayakuwa mageni kwao.

“Ni kawaida bosi. Umewahi kusikia kuhusu KPLC (yaani Kenya Power)? Huwa wanafanya mambo yasiyowezekana yawezekane,” aliandika Eugene wangs.

“Waaah bwana balozi kwani unaishi Kenya gani na jinsi stima hupotea kila wakati…ngoja ule wakati token zitaisha ukioga asubuhi,” Wanjiku alimpasha.

Pole sana bwana balozi. Umejiunga sasa na kilabu cha wanaokwamba kwenye lifti katika taifa letu. Karibu katika ulimwengu mpya,”Frank alisema

Baadhi walimkumbusha jinsi alivyokuwa na bahati kwamba Kenya hakukuwa na virusi hatari vya Homa ya China.

“Una bahati uko Nairobi na hakuna watu walioambukizwa Homa ya China ndani ya lifti,” alihoji Mohamed Abdi.

Wengine walimtahadharisha dhidi ya kutoroka kutokana na masaibu hayo.

“Ndio ututoroke tubaki tukipambana na Jubilee pekee yetu? La hasha, tuko pamoja katika safari hii,” Kachosi alieleza.

Balozi McCarter amejitahidi kujifahamisha na hali ya Wakenya na utampata akizungumza Kiswahili, sheng na hata kutangamana na wananchi katika vitongoji duni kama vile Kibera.