Michezo

Balozi wa Ghana aitaka Asante Kotoko iilipizie kisasi Black Stars

December 14th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

USHINDI wa Harambee Stars ya Kenya wa bao 1-0 dhidi ya Black Stars ya Ghana mwezi Septemba bado unauma Waghana na sasa Balozi wa Ghana nchini Kenya, Francisca Ashietey-Odunton ametaka Asante Kotoko ilipize kisasi itakapomenyana na Kariobangi Sharks hapo Jumamosi.

Sharks na Kotoko zinawania tiketi ya kusonga mbele katika Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup). Mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza kati ya klabu hizi mbili itasakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi saa tisa alasiri Desemba 15, 2018.

Timu hizi hazijawahi kukutana katika mashindano yoyote. Pia ni mara ya kwanza kabisa Sharks inashiriki mashindano yoyote ya Afrika tofauti na Kotoko ambayo ina uzoefu wa miaka 36.

Balozi Ashietey-Odunton ametembelea timu hiyo ikifanya mazoezi uwanjani Kasarani na katika ujumbe wake hakuficha matamanio yake kuona Waghana hao wanarejea nchini mwao na ushindi.

“Wacha niwaeleze kitu kimoja, mara ya mwisho timu kutoka Ghana ilizuru Kenya, tulilimwa. Timu hiyo ni Black Stars. Hii ni timu ya pili kutoka Ghana inayozuru hapa mwaka huu na ombi langu ni mlipize kisasi kichapo ambacho Ghana ilipata,” balozi huyo amenukuliwa na tovuti ya Asante Kotoko akisema.

Ameongeza, “Najua tuko hapa kupata ushindi na Jumamosi tutakuwa uwanjani kuwashabikia.”

Imebainika kwamba sababu za Kotoko kulalamikia mapokezi duni kutoka kwa Sharks ni kwamba wenyeji wao wamewapa basi ndogo la kusafirishia timu yake kutoka hoteli yao hadi uwanjani Kasarani. Pia wanadai walipewa uwanja wa Utalii Grounds mtaani Ruaraka ‘ambao viwango vyake ni vya chini kufanyia mazoezi’ kabla ya kupata fursa ya kutumia Kasarani. Kiingilio cha mechi hii ni Sh200 kwa maeneo ya kawaida ya uwanja na Sh500 kwa wageni mashuhuri.

Ushindi wa 1-0 dhidi ya Ghana mwezi Septemba uliweka Harambee Stars pazuri kurejea katika Kombe la Afrika (AFCON) tangu mwaka 2004. Wakenya kisha walikaba Ethiopia 0-0 ugenini na kuwachabanga 3-0 katika mechi ya marudiano jijini Nairobi na kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2019. Kenya na Ghana zitarudiana mjini Kumasi mwezi Machi mwaka ujao.