Makala

BAMBIKA: Posa zilizoduwaza

July 3rd, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

WAKATI maceleb wa hapa nyumbani wakionekana kupendelea kuwa na mahusiano ya kimya kimya na hata wanapotoa posa kwa wapenzi wao lazima iwe jambo la siri, majuu mambo ni tofauti kabisa.

Ukiwa Marekani, celeb kumposa mwenzake huwa ni tukio kubwa sana na la kutamanisha. Ili kudhihirisha mapenzi na nia yao, maceleb wa kiume huposa wapendwa wao kwa pete za bei ghali zilizosukwa na madini kama vile almasi, dhahabu, shaba kati ya zinginezo. Kwa mfano…

Rapa Kanye West pamoja na staa wa vipindi vya runinga Kim Kardashian wawasili mjini Los Angeles kuhudhuria makala ya 57 ya tuzo za Grammy Februari 8, 2015. Picha/ AFP

Kim Kardashian & Kanye West

Pete: Sh768 milioni

Baada ya kumtema mchezaji vikapu Kris Humphries, Kim alianza uhisiano na rapa Kanye ambaye kwa sasa ni mume wake. Ili kumdhihirishia penzi lake kwake kabla ya kumwoa 2014, Kanye alimposa Kim na pete iliyotengenezwa na madini karati 15 ya alamasi, lulu na dhahabu iliyomgharimu kiasi cha Sh768 milioni.

Beyonce & Jay Z

Pete: Sh480 Milioni

Wanamuziki hawa maaarufu kote duniani wamekuwa katika ndoa kwa takriban miaka 12 sasa tangu walipofunga pingu za maisha. Ikizingatiwa kuwa wote ni matajiri hasa rapa Jay Z anayeorodheshwa kuwa bilionea wa kwanza mwanamuziki, unaweza kuamini ni kwa nini haikuwa mzigo kwake kumvisha Beyonce pete ye uchumba ya thamani ya Sh480 milioni.

Jennifer Lopez & Marc Antony

Pete: Sh394 milioni

Mwigizaji na mwimbaji J Lo ametaliki wanaume watatu katika maisha yake ya ndoa hadi kufikia wakati huu. Cris Judd, Ojani Noa na Marc Anthony ndio wanaounda orodha hiyo.

Marc alioana na Lopez miezi michache baada ya mrembo huyo kutemana na aliyekuwa mchumba wake Ben Affleck waliyekuwa wameratibu kuoana Septemba 2003. Hata hivyo, waliahirisha tarehe ya harusi yao na kabla ingetimia walikuwa tayari wametemana.

Marc ambaye ni mwanamuziki alijizatiti kuuteka moyo wa Lopez kwa kumposa na pete iliyoundwa kwa madini ya dhahabu na almasi aliyoinunua kwa Sh394 milioni. Licha ya hilo ndoa yao haikudumu sana wakitalikiana 2005.

Anna Kournikova & Enrique Iglesias

Pete: Sh240 milioni

Mastaa hawa wamekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya miaka 13 sasa ila mpaka sasa hawajaonyesha pupa ya kutaka kufunga ndoa. Ijapokuwa wamejaliwa watoto watatu, Anna ambaye ni raia wa Urusi ni mchezaji tenisi mstaafu aliyetesa sana enzi za uchezaji wake huku mpenziwe akiwa ni mwanamuziki wa kusifika kutoka Uhispania.

Kwa sasa wanachumbiana ila bado hawajaamua ni lini wataooana. Pete iliyoundwa kwa karati ya madini 11 tofauti na iliyomgharimu Enrique Sh240 milioni ndiyo inayohalalisha uchumba wao.

Kim Kardashian & Kris Humphries

Pete: Sh192 milioni

Kwa sasa msoshiolaiti Kim ni mke halali wa ndoa kwa rapa mzushi wa Marekani Kanye West ambaye tayari kamzalisha watoto wawili North West na Saint West huku wengine wawili wakizaliwa na mama wa kukomboa.

Kabla ya ujio wa Kanye, Kim alichumbiwa na kuolewa na mchezaji wa mpira wa vikapu Humphries ambaye ndoa yao ilidumu kwa siku 72 pekee. Kidoleni alipokuwa akimposa, Kris alimvisha Kim pete iliyoundwa na mseto wa madini ghali, iliyomgharimu Sh192 milioni.

Ciara & Future

Pete: Sh144 milioni

Ciara ni mwanamuziki wa Rnb huku Future ambaye aliwahi kuwa mchumba wake akiwa ni mmoja wa marapa wakubwa wa Marekani. Ciara ambaye alijaliwa kupata mtoto kwa jina Future Zahir Wilburn na rapa huyo, aliamua kuvunja uchumba mwaka jana baada ya kugundua kuwa jamaa wake alikuwa akimega nje.

Kabla ya kuchukua hatua hiyo, Future alikuwa tayari kamposa kwa kumvisha pete iliyoundwa na madini 15 ya almasi iliyogharimu Sh144 milioni.

Katie Holmes & Tom Cruise

Pete: Sh144 milioni

Mapenzi ya waigizaji hawa wa Hollywood yalikuwa moto moto miaka 10 iliyopita. Kipindi hicho 2005 ndipo Cruise alijitengenezea jina na filamu zake za Mission Impossible. Alimposa Holmes jijini Paris Ufaransa, kwa pete ya dhahabu aliyoinunua kwa kitita cha Sh144 milioni. Wakati huo Cruise alikuwa na miaka 42, huku mpenziwe akiwa 26. Hata hivyo mapenzi yao yalidumu kwa miaka saba kabla ya kutalikiana 2012. Wawili hao wana binti mwenye umri wa miaka tisa.

Jennifer Lopez & Ben Affleck

Pete: Sh116 milioni

J-Lo alianza kutoka na mwigizaji Affleck 2002 na baada ya mwaka mmoja walipanga kulishana yamini Septemba 2003 lakini wakaahirisha tarehe na miezi michache penzi lao likatibuka. Miezi michache baadaye ndipo alipooana na Marc ambaye kamzalisha mapacha wawili, Emme na Max wenye umri wa miaka saba kwa sasa.

Unaweza kuelewa ni kwa nini Jenniffer alihisi uzito kumpoteza Ben Affleck kwani kwa hakika alimwonyesha penzi la kikweli ambalo hakuwa amewahi kulipata. Ben angemfanyia Jennifer chochote kile alichokitaka na ndio sababu haikuwa tatizo kwake kumposa na pete ya almasi iliyomgharimu kitita cha Sh116 milioni.

Jennifer Aniston & Justin Theroux

Pete: Sh99 milioni

Mwigizaji mashuhuri Aniston ambaye ni mke wa zamani wa Brad Pitt (tangu 2000 hadi 2005), amekuwa katika uhusiano na Theroux ambaye pia ni mwigizaji, mwongozaji na mwandishi wa filamu tangu 2012.

Justin ambaye anatamani sana kumwoa Aniston aliyeripotiwa kuahirisha siku ya harusi yao Machi mwaka huu, tayari kamposa kwa kumvisha pete iliyotengezwa na madini 10 ya alamasi iliyomgharimu Sh99 milioni. Kwa pamoja, wawili hawa wana utajiri unaokadiriwa kupita Sh13 bilioni.

Angelina Jolie & Brad Pitt

Pete: Sh48 milioni

Baada ya kuwa wapenzi kwa miaka tisa, waigizaji hawa vichwa wa Hollywood walifunga ndoa kirasmi mnamo Agosti 2014 nchini Ufaransa. Ukizingatia kwamba Brad na Jolie ni miongoni mwa waigizaji matajiri na wanaolipwa mshahara mkubwa na Hollywood, lazima tu posa ya mwanadada huyo ingekuwa yabei ghali.

Brad alichokifanya ni kumnunulia mpenziwe pete iliyotengenezwa na madini 16 ya almasi, iliyomgharimu dola nusu milioni kiasi ambacho ni sawa na Sh48 milioni. Hata hivyo, ni kiasi kidogo cha pesa ukizingatia kuwa Brad na Angelina kwa pamoja wana utajiri wa zaidi ya Sh41 bilioni.