Makala

BAMBIKA: Walivyotuacha kwa njia tatanishi

February 28th, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

JUMATANO wiki iliyopita, alizikwa msanii wa injili Papa Dennis kule kwao Matunda, Kakamega ikiwa ni wiki mbili baada ya kifo cha ghafla.

Papa Dennis aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha na kifo chake kimeendelea kuibua hisia mseto. Kuna mengi maswali kuliko majibu kuhusiana na alivyokumbana na mauti.

Lakini sio tu kifo chake ambacho kimewahi kuzua utata kuhusu kiini na chanzo, wapo wasanii wengine kibao tu ambao vifo vyao viliacha maswali mengi kuliko majibu. Hawa ni baadhi yao:

PAPA DENNIS (Februari 2020)

Ajirusha ghorofani?

Mwili wa Papa ulipatikana saa saba usiku nje ya jengo la orofa 12 kwenye mtaa wa Pangani, Nairobi. Inadaiwa kuwa Papa alijiua kwa kujirusha kutoka orofa ya saba baada ya kulemewa na stresi za maisha. Stresi hizo zimedaiwa zilianza baada yake kutemwa na lebo ya Maliza Umaskini inayomilikiwa na mfanyabiashara milionea Sadat Muhindi.

Chini ya lebo hiyo, Papa aliishi maisha ya anasa, ustaa na ufahari. Aliendesha magari ya nguvu na kupiga pamba za bei. Lakini mara tu alipotoka Maliza Umaskini iliyokuwa ikimpa maisha yao, Papa akasota. Nyumba aliyokuwa akiishi ikafungwa kutokana na yeye kushindwa kulipa kodi. Hapo akaanza kulala kwenye studio ya produsa Mash Mjukuu iliyoko Pangani jengo ambalo anadaiwa kujirusha kutoka juu. Hata hivyo, kinachotia utata ni namna kifo chake kilivyotokea.

Mwili wa Papa ulipatikana upande wa pili wa orofa hiyo ambapo hauna madirisha au balcony inakoweza kusemekana ndiko alisimama na kisha kujirusha. Ingelikuwa ni sehemu ya mbele basi ingeeleweka zaidi kutokana na kuwepo na balcony nyingi na madirisha. Picha hii imepelekea kuzuka kwa tetesi kwamba huenda aliuawa na kisha mwili wake kuburuzwa hadi upande wa pili.

PRINCE PAISLEY (April 2016)

Madawa ya kupunguza maumivu

Nyota huyu alifariki dunia akiwa na miaka 57 kwa kile kinachodaiwa kuzidisha dozi ya Opioid moja kati ya dawa zinazotumika kupunguza maumivu mwilini

Baada ya uchunguzi wa miaka miwili wapelelezi walisema hakuna mtu wa kushtakiwa kuhusiana na kifo cha Prince kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Wachunguzi walisema walikosa ushahidi ambao ungeelezea ni nani aliyempa dawa hizo ambazo zilipatikana kuwa na madini mengine ya sumu. Lakini hata zaidi walikosa ushahidi wa kuelezea ni vipi alipitiliza vipimo wakati huwa zina maelekezo ya kiwango cha kutumiwa.

BOBBI KRISTINA BROWN (Julai 2015)

Kokeni

Kifo cha binti huyu kilifanana sana na kile cha mamake marehemu nguli wa muziki Whitney Houston aliyepatikana akiwa hoi bafuni kwenye hoteli ya Beverly Hilton.

Upasuaji ulibainisha kwamba Whitney alifariki kutokana na madhara ya dawa ya kulevya ya kokeni aliyokuwa mraibu.

Miaka mitatu baadaye, bintiye wa pekee Bobbi akiwa na miaka 22 naye alipatikana nyumbani kwake bafuni kazama kwenye Jacuzzi akiwa hoi. Alikaa kwenye koma kwa miezi sita na hakuwahi kuamka.

Uchunguzi ulibaini kuwa alifariki kutokana na mchanganyiko wa madawa ya kulevya mwilini mwake huku akiwa amezama. Uchunguzi ulishindwa kubaini ikiwa ilikwa kifo cha makusudi au kilisababishwa na mtu. Mpenzi wake ambaye kwa sasa naye ni marehemu Nick Gordon alituhumiwa kwa kifo hicho.

BRUCE LEE (Julai 1973)

Uvimbe wa ubongo

Usiku mmoja, Bruce Lee, mmoja kati ya waigizaji bora wa aksheni kuwahi kutokea, alikwenda kulala na hakuamka. Inasemekana kifo chake kilisababishwa na uvimbe ghafla kwenye ubongo wake.

Lakini utata uliopo ni kwamba jamaa wakati wa kifo chake alikuwa fiti kiafya. Imedaiwa kuna uwezekano alimeza dawa za maumivu kabla ya kulala zilizosababisha uvimbe huo. Hata hivyo hamna ushahidi wa kuthibitisha hilo.

TUPAC SHAKUR (Septemba 1996)

Apigwa risasi

Miaka miwili kabla, kulikuwa na majaribio ya kumuua Tupac ambayo aliwalaumu wabishi wake Puff Daddy na Notorious BIG. Kifo chake kilitokea 1996 siku sita baada ya kupigwa risasi mara sita na watu wasiojulikana wakati akielekea kutumbuiza kwenye shoo moja mjini Las Vegas. Mpaka leo waliohusika kwenye kifo chake hawajawahi kujulikana wala kiini cha kumuua kilikuwa kipi haswa.

Hata hivyo, mashabiki wake wengi walishuku Notorious BIG huenda alihusika.

NOTORIOUS BIG ( Machi 1997)

Apigwa risasi

Miezi sita baada ya kifo cha Tupac, naye B.I.G alipigwa risasi mjini Los Angeles akiwa anatoka kwenye pati moja. B.I.G alikuwa kwenye gari lake pamoja na walinzi waliposimama, na ghafla akatokea mtu kwenye gari tofauti aliyeshusha kioo cha gari lao na kumiminia risasi gari la B.I.G. Alifariki dunia saa moja baada ya tukio hilo.

Mpaka leo hakuna aliyekamatwa. Kiini na chanzo cha kifo chake hakijulikani ila kimehusishwa na kifo chake Tupac hii ikitajwa kama ulipizaji kisasi. Kama tu Tupac hakuna aliyeshtakiwa.