Michezo

Bamford afunga matatu na kusaidia Leeds United kuzamisha chombo cha Aston Villa ligini

October 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LEEDS United walikomesha rekodi nzuri ya Aston Villa katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwapiga 3-0 katika ushindi uliomshuhudia fowadi Patrick Bamford akicheka na nyavu mara tatu.

Villa walishuka kwenye gozi hilo wakijivunia rekodi ya kusajili ushindi katika mechi nne za ufunguzi wa muhula wa huu wa 2020-21 ligini kwa mara ya kwanza tangu 1930-31. Ushindi kwa kikosi hicho cha kocha Dean Smith kungalishuhudia Villa wakipaa hadi kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 15.

Hata hivyo, umahiri wa Bamford kwenye safu ya mbele ya Leeds waliorejea EPL msimu huu baada ya miaka 16, ulizuia Villa kuweka rekodi ya kusajili ushindi katika mechi tano za kwanza ligini mfululizo.

Matokeo ya mechi hiyo iliyochezewa ugani Villa Park mnamo Oktoba 23, yalishuhudia Leeds wakichupa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali. Hiyo ndiyo nafasi bora zaidi kwa limbukeni hao wa EPL kuwahi kushikilia ligini tangu Septemba 2002.

Baada ya pande zote mbili kuambulia sare tasa kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Bamford aliwafungulia Leeds ukurasa wa mabao kunako dakika ya 55 baada ya kushirikiana na Jack Harrison aliyechangia pia la pili kunako dakika ya 67.

Sajili mpya wa Leeds, Moreno Rodrigo alipoteza nafasi nyingi za wazi dhidi ya Villa walioingia ugani wakijivunia motisha ya kupepeta mabingwa watetezi wa EPL, Liverpool 7-2 katika mchuano wao uliotangulia ugani Villa Park.

Licha ya Leeds kukosa huduma za nyota Kalvin Phillips na nahodha Liam Cooper wanaouguza majeraha, Villa walitepetea pakubwa na wakazidiwa maarifa na wageni wao katika idara zote.