Bandari: Azimio, KK wakwaruzana

Bandari: Azimio, KK wakwaruzana

NA ANTHONY KITIMO

TOFAUTI za kisiasa zimeanza kutishia juhudi za wakazi, mashirika ya kijamii na wanasiasa kushinikiza serikali irudishe haraka shughuli na huduma za Bandari zilizokuwa zimehamishwa.

Mizozano ya kisiasa ilitokea Jumatano wakati mashirika ya kijamii, wanasiasa na makundi ya kibiashara yalipokuwa yameitisha maandamano kwa dhamira ya kushinikiza Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) iharakishe kutekeleza agizo hilo lililotolewa na Rais William Ruto juma lililopita.

Maandamano hayo yalitamatika ghafla wakati kikundi kilichokuwa kimekusanyika katika makutano ya barabara ya Saba Saba, kutofautiana kuhusu mwanasiasa anayestahili kusifiwa kwa kumshawishi Rais Ruto.

Alipoapishwa, Dkt Ruto aliamrisha kuwa agizo la kulazimisha watu kusafirisha mizigo yao kwa reli ya SGR liondolewe na shughuli ya kukagua na kupitisha mizigo irudishwe Mombasa.

Waandalizi wa maandamano chini ya vuguvugu la Fast Action Business Community Movement walilazimika kuyatamatisha wakati wafuasi wa miungano ya Azimio na Kenya Kwanza walipoanza kuzozana.

“Tulikuwa tumepanga maandamano ya amani kumpongeza Rais Ruto kwa hatua yake na pia kushinikiza KPA itoe ilani kwa umma kuhusu utekelezaji wa amri ya Rais lakini tukatatizwa na wafuasi wa wanasiasa walioungana nasi,” akasema mwenyekiti wa vuguvugu hilo, Bw Salim Karama.

Wakati kikundi hicho kilipoanza kutawanyika ili kuzuia ghasia, polisi katika Bandari ya Mombasa walikaa macho kuzuia shughuli kutatizwa bandarini.

“Tunaomba wasimamizi wa KPA watangaze wazi kwamba waagizaji wa mizigo kutoka nchi za kigeni wako huru kujiamulia wanapotaka kupokea huduma na mbinu ya uchukuzi wanayotaka kutumia kusafirisha mizigo yao,” akasema Bw Karama.

Madalali wa kukagua na kupitisha mizigo nchini walisema KPA haijatoa ilani kuarifu waagizaji mizigo na wadau wengine kwamba huduma zimerudishwa Mombasa.

Mwenyekiti wa muungano wa Kenya International Forwarding and Warehousing Association (Kifwa), Bw Roy Mwanthi, alisema tangazo hilo likitolewa ndipo agizo la Rais Ruto litaweza kuanza kutekelezwa.

Kulingana na KPA, mipango bado inaendelezwa kuandaa jinsi agizo la Rais litakavyotekelezwa.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Garashi wahimizwa kujenga vyoo

Serikali yazindua rasmi mbolea ya bei nafuu

T L