Michezo

Bandari FC kuzuru S. Africa ikishinda Sharks Shield Cup

May 21st, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF na PHILIP ONYANGO

KLABU ya Bandari imeahidiwa kupata zawadi ya ziara ya wiki moja ya mazoezi nchini Afrika Kusini ikishinda mabingwa watetezi Kariobangi Sharks katika fainali ya SportPesa Shield mnamo Juni 1.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA), Daniel Manduku ambaye pia alitoa amri mishahara ya wachezaji pamoja na maafisa wa benchi la ufundi iongezwe kutoa motisha kwa timu.

Kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa timu hiyo katika hoteli moja mjini Mombasa jana, Manduku pia aliahidi kuinunulia timu hiyo basi la kisasa la kutumiwa kwa mechi za ugenini.

Alisema Bandari imefanya vizuri kwenye Ligi Kuu na SportPesa Shield na inastahili kupewa motisha ili iweze kutawala soka mkoani Pwani na Kenya kwa ujumla.

“Nimekuwa nikiangazia mechi zenu kimakini na nimekuwa nikipata habari zenu dakika hadi dakika mnapokuwa uwanjani mukicheza mechi na naweza kuwaambia kuwa mmekuwa mkicheza vizuri sana hata naamini kama si ratiba ya mechi kufuatana, mngeweza kuibuka mabingwa,” alisema Manduku.

Kulingana na Manduku, ambaye ni mlezi wa klabu hiyo, timu hiyo imekuwa ikitoa ushindani kwa timu zote na ana imani kubwa wakati utafika itaweza kumaliza utawala wa Gor kwenye.

“Nimekuwa nanyi na nitaendelea kuwa nanyi kwa sababu mmeweza kutamba si hapa nchini pekee, bali pia mmeweza kutamba hata nje ya nchi,” aliambia timu hiyo, huku akisifu jinsi magazeti ya Daily Nation, Taifa Leo na Mwanaspoti yalivyotambua maendeleo ya timu hiyo.

Aahidi kufika uwanjani Kasarani

Manduku aliahidi kufika mwenyewe uwanjani Kasarani jijini Nairobi kushangilia Bandari kwenye fainali dhidi ya Sharks ambapo vijana wa kocha Bernard Mwalala wameahidi kupata ushindi.

Katibu wa timu ya Bandari, Dickson Kibagendi, ambaye alikuwa akiongoza shughuli hiyo alikuwa amemwambia Manduku hapo awali kuwa wachezaji wanapania kulipiza kisasi cha kushindwa na Sharks kwenye fainali ya SportPesa Super Cup jijini Dar es Salaam nchini Tanzania mwezi wa Februari.

“Wachezaji wetu hawa wangali na kiu ya kulipiza kisasi baada ya kufungwa 1-0 na Kariobangi Sharks katika fainali nchini Tanzania, lakini tumewashinda nyumbani Mombasa na ugenini Nairobi ligini. Tuna tamaa kubwa ya kushinda taji hili Juni 1,” alisema Kibagendi.

Mshindi kati ya Bandari na Sharks ataingia soka ya Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup) ya msimu 2019-2020.

Manduku pia alitoa ahadi ya kutafuta njia za kuongeza motisha ya wachezaji wa timu za mchezo wa mpira wa vikapu za wanaume na wanawake zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.