Bandari FC yatoka sare na AFC Leopards

Bandari FC yatoka sare na AFC Leopards

Na STEVEN HEYWOOD

TIMU ya Bandari imeponyoka na pointi moja dhidi ya mahasimu wao wa jadi AFC Leopards katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya iliyogaragazwa ugani Nyayo, Jumapili alasiri.

Bandari ilipata goli la kwanza kupitia mshambuliaji Yohana Mwita katika dakika 19 kabla ya Maxwell Omondi kusawazisha katika dakika ya 28.

Mchezaji wa Harambe Stars Abdallah Hassan aliipatia Bandari bao la pili katika dakika ya 40 lakini matunda hayo yaligawanywa kati kwa kati baada ya Marvin Nabwire kusawazisha katika dakika za lala salama.

Kocha mkuu wa Bandari FC Antony ‘Modo’ Kimani amesema kwamba mechi mbili alizocheza akiwa amevikwa majukumu ya kocha mkuu hazijakuwa rahisi lakini ana matumaini kwamba timu yake itazidi kunoa makali katika mechi zijazo.

“Mechi zinazidi kuwa ngumu na wakati huu kila mtu anang’ang’ania pointi ali aweze kumaliza nafasi nzuri zaidi mwisho wa ligi. Sisi tunachukua kila mechi kama fainali na tutazidi kujinoa ili tumalize tunakofaa,” akasema kocha wa Bandari.

Bandari wana kibarua kigumu wiki hii kwani wako ugenini dhidi ya Talanta, Jumatano hii, na wamesalia namba nane katika jedwali la Ligi Kuu ya Kenya.

Kocha mkuu wa AFC Leopards, Patrick Aussems aliisifu timu yake kwa kuokota pointi moja hiyo.

“Nadhani nyote mwajua hali ilivyo hapa AFC Leopards na wachezaji wangu wanapitia dhiki kubwa sana lakini nawashukuru kwa kupata pointi moja hiyo,” amesema kocha huyo.

AFC wamekwama katika nafasi ya 10 na wanapambana na Ulinzi katika mechi ijayo.

You can share this post!

Aliyenaswa na bangi ya Sh25m kushtakiwa

Baadhi ya takwimu za kurejelea mafanikio ya Jubilee...

T L