Michezo

Bandari na Sharks ndani ya fainali ya kumenyana na Everton

January 25th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

FAINALI ya soka ya kimataifa ya SportPesa Super Cup mwaka 2019 itakutanisha Bandari na Kariobangi Sharks baada ya klabu hizi kutoka Kenya kukanyaga Watanzania Simba SC na Mbao FC jijini Dar es Salaam, Ijumaa.

Bandari ilijikatia tiketi kwa kushinda nusu-fainali ya kwanza kwa kuchapa Simba 2-1 nayo Sharks ikabwaga Mbao kwa njia ya penalti 6-5 baada ya muda wa kawaida kutamatika 0-0. Timu hizi za Kenya zitavaana katika fainali mnamo Januari 27.

Washiriki wapya kabisa Bandari katika soka hii ya klabu nane kutoka mataifa ya Kenya na Tanzania hawakupata ushindi kwa urahisi.

Walitoka chini bao moja na kulipua Simba kupityia mabao ya William Wadri na Wilberforce Lugogo.

Mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia, Meddie Kagere alipeleka Simba mapumzikoni bao 1-0 mbele baada ya kuona lango sekunde chache kabla ya dakika 45 za kwanza kutamatika.

Abdalla Hassan aliipa Bandari nafasi ya kusawazisha pale alipoangushwa ndani ya kisanduku cha Simba.

Mganda Wadri hakukosea kufuma wavuni penalti hiyo iliyopatikana dakika ya 59. Lugogo kisha alifungia Bandari bao la ushindi dakika ya 72 baada ya kocha Bernard Mwalala kumpa fursa ya kuonyesha uwezo wake alipomwingiza kama nguvu-mpya katika kipindi cha pili. Itakumbwa kwamba Wadri pia alifungia Bandari penalti safi katika kipindi cha pili iliyozamisha Singida United katika mechi ya ufunguzi mnamo Januari 22.

Nayo Sharks ilianza kampeni yake kwa kulipua Young Africans ya Tanzania almaarufu Yanga 3-2 mnamo Januari 22. Duke Abuya alifungia Sharks mabao mawili katika mchuano huo, huku Mganda George Abege akichangia bao moja. Sharks, hata hivyo, ilitolewa kijasho chembamba katika nusu-fainali ikiponea mara kadhaa kufungwa katika muda wa kawaida kabla ya kutawala upigaji wa penalti.

Ilianza kwa kupoteza penalti yake ya kwanza iliyochotwa na Patilah Omotto kabla ya kufunga kupitia Tom Teka, Sven Yidah, Geoffrey Shiveka, Nixon Omondi, Eric Juma na Michael Bodo. Nayo Mbao ilifunga penalti zake tatu za kwanza ikapoteza ya nne na kisha kufunga mbili zilizofuata kabla ya kupoteza ya sita

Miamba wa Kenya, Gor Mahia na AFC Leopards waliaga mashindano katika mechi yao ya kwanza. Gor, ambayo ilishinda makala ya mwaka 2017 na 2018, ililemewa na Mbao katika upigaji wa penalti 4-3 baada ya muda wa kawaida kutamatika 1-1. Leopards, ambayo ilifika fainali mwaka 2017 na kuondolewa katika hatua ya kwanza mwaka 2018, ilibanduliwa nje na Simba baada ya kulimwa 2-1.

Mshindi wa soka hii hupata fursa ya kupimana nguvu dhidi ya Everton kutoka nchini Uingereza. Gor ilichapwa 2-1 na Everton mwaka 2017 jijini Dar es Salaam kabla ya kupondwa 4-0 uwanjani Goodison Park nchini Uingereza mwaka 2018. Mshindi wa makala haya ya tatu pia atasafiri nchini Uingereza kumenyana na Everton baadaye mwaka huu kwa hisani ya kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa, ambayo ndiyo mdhamini na mwanzilishi wa soka hii. SportPesa pia inadhamini Gor, Leopards, Simba na Yanga na Everton.