Michezo

Bandari, Sofapaka ni toka nipite wakiwania namba 2

May 21st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABADILIKO sita yameshuhudiwa kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ambayo Gor Mahia inaongoza bila presha kutoka kwa mpinzani wa karibu Bandari baada ya mechi 31 kusakatwa, wikendi.

Mabingwa watetezi Gor wananusia taji lao la tatu mfululizo na 18 kwa jumla ya alama 69 baada ya kunyamazisha mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards kwa mabao 3-1 Jumapili.

Bandari iliepushia washindi mara 13 Leopards aibu ya kufanyia Gor gwaride la heshima ilipokanyaga Zoo Kericho 3-0, na hivyo kusalia alama nane nyuma ya vijana wa Hassan Oktay.

Baada ya kumaliza mechi mbili bila ushindi, washindi wa mwaka 2009 Sofapaka wameachwa kwa alama nne na Bandari, ingawa wamesalia katika nafasi ya tatu.

Vilevile, Kakamega Homeboyz hawajasonga kutoka nafasi ya nne baada ya kujiongezea alama moja kutokana na sare tasa dhidi ya Posta Rangers.

Homeboyz na Sofapaka, ambazo zimevuna alama 52 na 57 mtawalia, ndizo zinazojivunia wachezaji wanaofukuzana vilivyo katika vita vya kutoa mfungaji bora.

Allan Wanga anaongoza ufungaji wa mabao baada ya kucheka na nyavu mara 18 naye Mganda Umaru Kasumba yuko goli moja nyuma baada ya kupachika bao lake la 17 Sofapaka ilipotoka 1-1 dhidi ya Nzoia Sugar.

Mabingwa wa mwaka 2006 SoNy Sugar wameruka juu nafasi moja na kutua katika nafasi ya tano baada ya kulima Mount Kenya United 3-1.

Wanasukari hawa wamezoa alama 52. Wamesukuma washindi wa mwaka 2008 Mathare United nafasi moja chini hadi nambari sita. Mathare ilikabwa 0-0 dhidi ya Western Stima ugenini.

Badiliko halikushuhudiwa katika nafasi ya saba pale mabingwa mara 11 Tusker waliposalia katika nafasi hiyo baada ya kulemea Vihiga United 2-1. Wanamvinyo hawa wana alama 49.

Wanabenki wa KCB ndio waliimarika zaidi katika raundi ya 31.

Ushindi wao wa mabao 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks uliwapaisha kutoka nafasi ya 11 hadi nambari nane. KCB imezoa alama 40.

Imezidia nambari tisa Ulinzi Stars kwa tofauti ya magoli. Wanajeshi wa Ulinzi walitoka Chemelil na alama moja baada ya kukaba Chemelil Sugar 0-0.
Leopards almaarufu kama Ingwe, ambayo imeambulia alama mbili katika mechi tano zilizopita, inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 39. Ulinzi na Ingwe zilishuka nafasi moja kila mmoja.

Sharks chini nafasi moja

Vilevile, Sharks sasa iko chini nafasi moja hadi nambari 11 baada ya kupokea vichapo viwili mfululizo.

Nzoia, Stima, Rangers na Chemelil zimesalia katika nafasi ya 12, 13, 14 na 15 baada ya kupiga sare kila moja na kufikisha alama 37, 32, 31 na 30 mtawalia.

Zoo na Vihiga zilipata pigo katika juhudi zao za kujiondoa katika maeneo hatari ya kutemwa baada ya kupoteza mechi zao. Zoo ina alama 28.

Inashikilia nafasi ya 16, ambayo ni timu itakayokamliza katika nafasi hiyo itakayomenyana na nambari tatu kutoka Ligi ya Supa kuamua itakayoshiriki Ligi Kuu 2019-2020.

Vihiga ni ya 17 kwa alama 25. Mount Kenya ilitemwa baada ya mechi za raundi ya 31 kwa sababu alama nyingi inayoweza kukusanya ikishinda mechi tatu zilizosalia msimu huu ni 27. Ilipoteza mechi yake ya tano mfululizo ilipocharazwa na SoNy.