Michezo

Bandari waamini hatima yao ni leo Jumamosi wakisaka Betway

March 14th, 2020 1 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MATOKEO ya mechi ya Kombe la FKF (Betway) baina ya Bandari na Sofapaka FC itakayopepetwa uwanjani Mbaraki Sports Club leo Jumamosi, ndiyo yatakayoamua hatima ya Bandari FC katika mechi zilizosalia msimu huu.

Kocha wa Bandari FC, Twahir Muhiddin amekumbusha kuwa alisema hapo awali kuwa mechi mbili dhidi ya wapinzani wao wakubwa wa Kariobangi Sharks na Sofapaka ndizo zitakazoamua jinsi timu yake itakavyofanya katika sehemu ya mwisho ya msimu huu wa 2019-2020.

“Tumemaliza mechi yetu na Sharks na tumepata ushindi, sasa tunasubiri matokeo ya mechi yetu ya Jumamosi tutakayopambana na Sofapaka; hapo ndipo tutafahamu kama tumepiga hatua ya maendeleo ama tuko pale pale tulipokuwa,” akasema Muhiddin.

Bandari inapambana na Sofapaka kwenye mechi muhimu ya taji hilo la FKF ambalo timu zinapigania ili mshindi awakilishe nchi katika kandanda ya baraba (CAF) Confederation Cup.

Muhiddin alisema njia ya mkato kwa timu kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika ni kushinda taji la FKF Cup ambalo Bandari wanalishikilia na ambapo wamepania kulihifadhi.

Muhiddin alisema wanauchukulia mchezo wao wa leo kwa umuhimu mkubwa na amewataka wachezaji wake wacheze kufa kupona kuhakikisha wamepata ushindi ili kujiongezea matumaini ya kuweza kushinda tena taji hilo kwa mwaka wa pili mfululizo.

“Tunataka kwa vyovyote vile tuhakikishe tumewashinda wapinzani wetu hao kutoka Nairobi amvbao ni wagumu. Wanasoka watacheza kwa kujitolea na bidii zao zote kuhakikisha tunatoka uwanjani na ushindi,” akasema mkufunzi huyo.

Alisema jambo la kufurahisha ni kuwa beki wake Duncan Otewa amefanya mazoezi magumu na wenzake na anatarajia kuwemo katika kikosi cha hivi leo hali watasubiri uamuzi wa daktari kama watawaruhusu Abdalla Hassan na Shaaban Kenga kucheza mechi hiyo.