Michezo

Bandari wadhibiti usukani, Ingwe na Vihiga zikipaa KPL

March 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards na Vihiga United ziliimarika zaidi baada ya mechi za raundi ya 17 Jumapili ambapo klabu hizi zenye ufuasi mkubwa kutoka Magharibi ya Kenya zilijitoa katika mduara hatari wa kutemwa na kuruka juu nafasi mbili kila mmoja.

Bandari na Mathare United wanasalia katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 32 na 31 baada ya kusakata mechi 16 na 17 mtawalia.

Viongozi Bandari walitamatisha mechi mbili bila ushindi walipolazwa 2-1 na Ulinzi Stars nao Mathare, ambao wamemaliza mechi zao za mkondo wa kwanza, pia walikamilisha mechi mbili mfululizo bila ushindi baada ya kutoka 0-0 dhidi ya Western Stima.

Sofapaka wamepiga hatua moja mbele hadi nafasi ya tatu. Walilipua Chemelil Sugar 3-0.

Vijana wa kocha John Baraza wamezoa alama 30 kutokana na mechi 17. Wamesukuma mabingwa watetezi Gor Mahia nafasi moja chini hadi nambari nne.

Gor wamekusanya alama 29 baada ya kucheza mechi 14 pekee. Vijana hawa wa Hassan Oktay watang’oa Bandari kileleni wakilima Kakamega Homeboyz katika mechi yao ijayo kwa sababu wana tofauti nzuri ya magoli.

Kariobangi Sharks wamerukia nafasi ya tano baada ya kuokota alama moja muhimu ugenini dhidi ya Posta Rangers katika sare ya 0-0. Wamesukuma mabingwa mara 11 Tusker chini nafasi moja hadi nambari sita.

Sharks na Tusker wamezoa alama 26 na 25 mtawalia. Wote wamesakata mechi 16. Tusker imepoteza mechi nne mfululizo. Ilipoteza 2-1 dhidi ya Leopards.

Iko mbele ya nambari saba SoNy Sugar kwa ubora wa magoli. Wanasukari wa SoNy walizaba Mount Kenya United 1-0 katika mechi yao ya 17. Stima, ambayo imeambulia sare tatu na kichapo kimoja katika mechi nne zilizopita, inasalia katika nafasi ya nane.

Imejizolea alama 23 kutokana na mechi 16. Wanaumeme hawa wako alama mbili mbele ya nambari tisa Homeboyz, ambayo haikuwa na mechi wikendi, na nambari 10 Ulinzi.

KCB yaichapa Nzoia Sugar

Wanajeshi wa Ulinzi walipaa nafasi moja na kusukuma Nzoia Sugar chini nafasi moja hadi nambari 11.

Nzoia ilisalia na alama 20. Ilichapwa 2-0 na KCB. Wanabenki wa KCB, ambao wamesakata mechi 17, moja zaidi ya Nzoia, wanasalia katika nafasi ya 12 kwa alama 19.

Posta na Leopards almaarufu Ingwe zimerukia nafasi za 13 na 14 kwa alama 16 kila mmoja baada ya kucheza mechi 17 na 16, mtawalia.

Vihiga imepaa kutoka nambari 17 hadi 15. Ilipepeta Zoo 2-1. Zoo iliathiriwa vibaya zaidi na kuimarika kwa Rangers, Ingwe na Vihiga.

Imeshuka chini nafasi tatu hadi nambari 16. Ina alama sawa na Vihiga 15, lakini zinatofautiana kwa ubora wa mabao.

Chemelil iko chini nafasi mbili hadi nambari 17 kwa alama 14 kutokana na mechi 16 nayo Mount Kenya imekamilisha nusu ya kwanza ya ligi hii ya klabu 18 mkiani alama mbili nyuma.