Habari Mseto

Bandari ya Kenya yalenga viwango vya kimataifa

August 13th, 2018 2 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

HALMASHAURI ya Bandari nchini (KPA) imeanza kuwekeza na kuifanya bandari ya Mombasa kuwa bora barani Afrika katika miaka miwili ijayo.

Mkurugenzi mkuu wa KPA, Bw Daniel Manduku alisema kuwa shirika hilo lenye thamani ya mabilioni ya fedha litategemea sana kuimarika kwa biashara katika bandari ya Mombasa kufikia malengo hayo.

Akiongea katika hoteli ya English Point Marina mjini Mombasa wakati wa dhifa iliyoandaliwa na bodi ya Vision 2030, alisema bandari hiyo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi mizigo kufikia tani milioni mbili.

“Katika bandari, tumelenga takribani maeneo manne ya kuwekeza ili kuhakikisha kwamba bandari ya Mombasa inaibuka bora katika bara la Afrika.

Yote haya tunafanya tukilenga ndoto ya Vision 2030 ambayo inahimiza kwamba taifa liwe limestawi katika kila nyanja kufikia mwaka wa 2030,” akasema Dkt Manduku. Alisema kwa sasa jambo la kwanza ambalo wamefanya ni kuboresha usimamizi wa bandari ya Mombasa.

“Jambo la pili ambalo tumefanya ni kuongeza nguvu kazi na kwa muda wa miezi miwili ambayo imepita, bandari ya Mombasa imevunja rekodi nne za uliwengu kwa kupakuwa na kuondoa mizigo kwa upesi.

Hii sio bandari tu ila tunataka kuwa bandari nambari moja kwa huduma bora zaidi barani Afrika.

Ninataka kuwahakikishia hapa kwamba ndani ya muda wa miaka miwili ijayo, bandari ya Mombasa itakuwa bandari bora zaidi katika bara la Afrika,” akasema.

Mkurugenzi huyo alisema wanaangalia sana sasa kuhusu kupanua biashara , jambo ambalo alisema litawezekana kupitia kwa kuwatia motisha wafanya kazi pamoja na kuwapa fursa nzuri ya kutumia taaluma zao kuongeza uzalishaji katika bandari.

“Tunalenga kuifanya bandari ya Mombasa iwe ya kisasa, na zaidi ya hayo tunataka kuona kwamba huduma zetu sasa zinahamia kwa asimilia mkubwa katika mfumo wa elektroniki,” akasema.

Baadhi ya miradi ambayo kwa sasa halmashauri hiyo infanya ni kama vile ujenzi wa bandari ya Lamu huku pia KPA ikilenga kupanua na kuboresha baadhi ya bandari nyingine katika kaunti ya Kisumu na Kwale.

“Kwa sasa tunamalizia ujenzi wa bandari ya Lamu ambayo ni mojawapo ya asasi ambazo zitakuwa chini ya uangalizi wetu wa moja kwa moja.

Tuko pia kwa sasa katika mpango wa kubadilisha kifungu cha sheria za bandari ili kuwezesha ujenzi zaidi wa bandari chini ya uangalizi wetu. Hii ni kwa sababu kile kifungu cha katiba cha mwaka wa 1978 kilizuia baadhi ya miundo msingi kutekelezwa,” akasema Dkt Manduku.

Baada ya kumalizika kwa ujenzi wa bandari ya Lamu, KPA itaanza ujenzi wa bandari ya Shimoni kabla ya kuelekea katika eneo la Kisumu ili kupanua bandari hiyo.

“Katika eneo la Kisumu, tayari tumepata ardhi na kwa sasa tunaendelea kuangalia miundo na ramani mbalimbali kabla tuchague ni muundo gani ambao utaendana kibiashara na bandari hiyo.

Vile vile tunalenga kupanua egesho la makasha la Nairobi (ICD) ambalo kwa sasa linapata mizigo kwa wingi kutoka bandari ya Mombasa,” akasema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa sasa, jumla ya makasha 8,000 huwa yanasafirishwa kwa bogi la SGR kutoka bandarini Mombasa.

“Kwa sasa tunasafirisha makasha 8,000 lakini tunapanga kufikia makasha 12,000 kufikia mwezi wa Disemba. Kwa sababu nafasi ni ndogo tumeamua pia kupanua egesho hilo la Nairobi,” akasema.

Bandari hiyo ya Kilindini pia sasa imeanza awamu ya pili ya ukarabati wa egesho nambari 21 kupitia kwa ufadhili wa shirika la JICA kutoka Japan.

“JICA ilikarabati maegesho 20 na 19 hapo awali na kwa sasa pia wanatusaidia kuboresha egesho 21, na ujenzi wake unaanza mwezi ujao.Vile vile maegesho ya zamani kuanzia egesho 11-15 pia yatarabatiwa kwa sababu yamechoka.

“Tunatarajia biashara itaimarika na lengo kamili ni kutaka kuona kwamba tunatoka katika kiwango cha hifadi ya mizigo cha tani 30 millioni hadi tani 45 kufikia mwisho wa mwaka huu,” akasema.