Michezo

Bandari yaalikwa kwa SportPesa Cup

November 15th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya mwaka 2015, Bandari FC wamepata mwaliko kushindania ubingwa wa makala yajayo ya SportPesa Cup yatakayofanyika Januari 22-27, 2019.

Wadhamini, kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa, pia wamealika Mbao FC kutoka Tanzania kushiriki makala hayo ya tatu. Bandari inachukua nafasi ya Kakamega Homeboyz nayo Mbao inajaza nafasi ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kutoka Zanzibar.

Gor Mahia ya kocha Dylan Kerr ilishinda makala ya kwanza yaliyojumuisha pia mahasimu wao wa tangu jadi AFC Leopards pamoja na Tusker na Nakuru AllStars (Kenya), klabu za Tanzania za Young Africans (Yanga), Simba SC na Singida United na Jang’ombe kutoka Zanzibar.

Vijana wa Kerr walihifadhi taji mwaka 2017. Makala ya pili yalivutia Gor Mahia, AFC Leopards, Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz (Kenya), Yanga, Simba na Singida (Tanzania) na JKU (Zanzibar).

Kila timu inayoshiriki mashindano haya ya muondoano huzawadiwa fedha. Nambari moja hadi tatu hupata Sh3,097,800, Sh1,032,600 na Sh774,450, mtawalia. Nambari nne hupokea Sh516,300.

Timu zinazoondolewa katika robo-fainali hutuzwa Sh258,150 kila mmoja. Bingwa wa SportPesa Cup pia hupata tiketi ya kumenyana na klabu ya Everton kutoka nchini Uingereza. Gor ilichapwa 2-1 na Everton jijini Dar es Salaam, Tanzania, mwaka 2017. Ilipepetwa 4-0 uwanjani Goodison Park mwaka 2018.