Bandari yafurahia uteuzi wa wachezaji wake wawili kuwajibikia Harambee Stars

Bandari yafurahia uteuzi wa wachezaji wake wawili kuwajibikia Harambee Stars

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BANDARI FC imefurahia kuona wanasoka wake wawili wakiwa miongoni mwa wachezaji katika kikosi cha timu ya taifa Harambee Stars itakayokabiliana na Sudan Kusini na Tanzania kwenye mechi za kirafiki za kimataifa.

“Tunajivunia Bandari FC yetu kuwa na mchezaji mwingine, Danson Namasaka kujumuishwa katika timu ya taifa akiwa pamoja na kiungo wetu mwingine Abdalla Hassan walioripoti kambi ya mazoezi hapo hoteli ya Utalii jana,” akasema meneja wa timu hiyo, Albert Ogari.

Ogari anasema wanashukuru maafisa wa benchi la ufundi la timu ya taifa kumuona Namasaka kuwa mwanasoka mwenye kipaji cha hali ya juu na wakamchagua kuwa katika kikosi cha timu inayojumuisha wachezaji wa kuwakilisha taifa kwenye mechi za kimataifa.

“Klabu yetu ya Bandari inajivunia kutoa mchezaji wake mwengine kwa timu ya taifa na mashabiki wanakubali kuwa Namasaka anastahili kuteuliwa na kuichezea timu hiyo Harambee Stars sababu ameonyesha kiwango cha juu cha uchezaji wake,” akasema Ogari.

Meneja huyo alisema anatarajia wachezaji wao hao wawili, wote wanaocheza nafasi ya kiungo, wataweza kuwafanya wateuzi wawachezeshe kwenye mechi hizo mbili dhidi ya Sudan Kusini na Tanzania.

“Nina matarajio makubwa Hassan na Namasaka watakuwemo katika kikosi kitakachokabiliana na Sudan Kusini na Taifa Stars ya Tanzania. Kuwako kwao katika Stars kutasaidia kuimarisha kikosi cha timu yetu kuwa na wachezaji wenye uzoefu,” akasema Ogari.

Kutokana na timu ya taifa kujiandaa kwa mechi hizo za kimataifa, mechi ya Bandari FC ya ugenini iliyokuwa ichezwe jijini Nairobi dhidi ya Wazito FC imeahirishwa na sasa imepangwa kuchezwa Machi 20 .

“Wanasoka wetu wengine wanaendelea na mazoezi kama kawaida chini ya Kocha Andre Cassa Mbungo na naibu wake Anthony Kimani kwa ajili ya kujitayarisha kwa mechi yetu hiyo ya ugenini ya Machi 20 ambayo tuna hamu tupate ushindi,” akasema.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally amepongeza uteuzi wa Namasaka na Hassan kwa timu ya taifa na amependekeza mabeki watatu, Siraj Mohamed, Brian Otieno na Bernard Odhiambo nao wapewe fursa ya kujaribiwa kikosi cha Stars.

You can share this post!

MKU na UNITAR zaingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa...

Badminton Kenya yapigwa marufuku baada ya mivutano ya...