Bandari yajiandalia Tusker, mastaa wanne kukosa mechi

Bandari yajiandalia Tusker, mastaa wanne kukosa mechi

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

BANDARI FC ilirudi Mombasa, jana Jumanne kutoka Nairobi ilikopata sare ya 1-1 na Wazito FC, huku kocha Andre Cassa Mbungo akiahidi kuzidi kunoa safu ya ushambuliaji kabla mechi ya Tusker wiki ijayo.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Mbungo amesema masogora wake walicheza soka nzuri lakini mastraika wakakosa nafasi kadhaa ambazo zingeliwapa ushindi katika pambano hilo la ligi.

“Tulitawala vizuri mchezo na hatukustahili kugawanya pointi ila kwa kukosa mabao mengi ya kufunga. Hii ndio safu nitaifanyika kazi kuanzia sasa hadi Jumanne ijayo, ili Jumatano tutakapocheza na Tusker ugenini mastraika waweze kutumia nafasi zao kufunga,” alisema.

Mkufunzi huyo wa Bandari amesema kuwa atafanya bidii kuhakikisha safu hiyo inafanya kazi na wachezaji wanapopata nafasi wanazitumia na kufunga mabao.

“Ninaamini tutakapokutana na Tusker tutakuwa imara zaidi na tunaweza kupata ushindi,” akasema na kufichua kuwa atakosa wachezaji wake wanne walioumia katika mechi zilizopita.

Hapo ni viungo Wyvonne Isuza aliyesajiliwa kutoka Wazito, Faraj Ominde aliyekuwa na Tusker na Keegan Ndemi na straika Umaru Kasumba.

“Tunao majeruhi hao ambao hatuna tamaa kama wanaweza kuwahi mechi ya Tusker lakini Isuza na Ominde watakosa mechi nyingi zaidi kutokana na majeruhi mabaya waliyoyapata,” akasema kocha huyo.

Albert Ogari ambaye ni meneja wa timu hiyo ya pekee ya Pwani katika ligi kuu anasema wanatarajia kuondoka Mombasa kuelekea Nairobi siku ya Jumapili na kufanya mazoezi siku mbili kabla ya pambano lao na Tusker siku ya Jumatano.

You can share this post!

Akida arejea Starlets, Alumirah akitaja kikosi cha muda

Serikali yaondoa kafyu ikihimiza raia kutahadhari

T L