Michezo

Bandari yang’oa Mathare United kileleni

January 17th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BANDARI FC imedumisha rekodi yake ya kutoshindwa na Posta Rangers hadi mechi saba baada ya kuandikisha ushindi wake wa pili mfululizo dhidi ya wapinzani hawa kwa kuwanyuka 1-0 mjini Mombasa, Alhamisi.

AFC Leopards pia ilipata ushindi wake wa pili mfululizo dhidi ya Chemelil Sugar baada ya kuipiga 2-1 mjini Chemelil katika mechi nyingine iliyosakatwa Alhamisi, huku Zoo ikimaliza mechi yake ya tano bila kupoteza dhidi ya Kariobangi Sharks pale ilipoikaba 1-1 mjini Kericho.

Bandari imerukia juu ya jedwali kutoka nafasi ya pili baada ya kupata bao muhimu katika dakika ya 56 kupitia shuti kali kutoka mbali kutoka kwa Abdallah Hassan, ambaye sasa amefunga katika mechi tatu zilizopita.

Imeng’oa mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United kutoka kileleni. Bandari ina alama 18 kutokana na ushindi tano na sare tatu nayo Mathare imeshuka chini nafasi moja alama mopja nyuma. Mathare haijasakata mechi yake ya nane.

Sharks pia imeimarika kutoka nafasi ya nne hadi nambari tatu baada ya kuambulia alama moja kutoka ziara yake ya Kericho. Ina jumla ya alama 14 kutokana na ushindi tatu na sare tano.

Bernard Odhiambo aliweka Zoo mbele 1-0 dakika ya 31 kabla ya Sharks kusawazisha kupitia kwa Yidah Sven Yidah dakika ya 89. Bandari, Mathare na Sharks ndizo klabu pekee hazijashindwa katika ligi hii ya timu 18.

Western Stima, ambayo ilishikilia nafasi ya tatu kwa alama 14 kutokana na mechi saba, imeteremka hadi nafasi ya nne kwa tofauti ya magoli.

Mabingwa watetezi Gor Mahia wanafunga mduara wa tano-bora kwa alama 13 baada ya kuzaba Mount Kenya United 4-1 Jumatano. Ina alama 13 sawa na nambari sita Tusker nayo Leopards imeruka Kakamega Homeboyz, Ulinzi Stars, Nzoia Sugar na SoNy Sugar na kutua katika nafasi ya saba baada ya kulemea Chemelil kupitia mabao ya Jaffery Odeny na Eugene Mukangula. Ingwe, ambayo ilikuwa imeshinda mechi moja tangu msimu uanze, imeimarisha alama zake hadi 10 kutokana na mechi nane.

SoNy ina alama tisa kutokana na mechi saba nazo Nzoia na Ulinzi zinashikilia nafasi za tisa na 10 kwa alama tisa kila mmoja kutoka na mechi sita na saba, mtawalia.

Homeboyz ina alama saba kutoka mechi saba. Sofapaka, Vihiga United, Chemelil na Zoo zinafuatana kutoka nafasi ya 12 hadi 15 kwa alama saba kila mmoja, ingawa Chemeli na Zoo zimesakata mechi moja zaidi.

Rangers inashikilia nafasi ya 16 kwa alama sita kutokana na mechi nane nazo KCB na Mount Kenya zimezoa alama tano na mbili katika nafasi mbili za mwisho.

Bandari, Sharks, Leopards na Gor zinatarajiwa kuondoka nchini mwisho wa juma hili kuelekea nchini Tanzania kwa mashindano ya kimataifa ya SportPesa Super Cup yatakayofanyika kutoka Januari 22-27.

Mshindi wa soka hii itakayokutanisha Wakenya dhidi ya Watanzania Singida, Yanga, Simba na Mbao, atajikatia tiketi ya kumenyana na Everton nchini Uingereza baadaye mwaka huu.