HabariSiasa

Bandari yapandisha joto la siasa

June 24th, 2020 2 min read

JUMA NAMLOLA na WACHIRA MWANGI

HATUA ya Serikali kuhamisha shughuli nyingi za bandari hadi miji ya Nairobi na Naivasha, imezua joto la kisiasa Pwani huku wanaharakati wakianzisha kampeni ya kuwatimua wabunge wawili.

Wabunge hao, Mishi Mboko wa Likoni na Ali Mbogo wa Kisauni wamewakasirisha wakazi wa Pwani kwa kupinga hoja ya mwenzao wa Nyali, Mohamed Ali ya kumwondoa Waziri wa Uchukuzi James Macharia madarakani, kwa hatua ambazo amesema zinavuruga uchumi wa Mombasa na Pwani kwa jumla.

Bi Mboko jana alipuuza hatua ya shirika la kijamii kuanza kukusanya sahihi kwenye mchakato wa kumwondoa yeye na Bw Mbogo, kwa madai ya kuwasaliti Wapwani akidai hoja ya kumwondoa Bw Macharia inachochewa kisiasa.

Hii ni baada ya vuguvugu la wafanyibishiara la Fast Action kufika katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuchukua hati ya kuliruhusu kukusanya sahihi za kuwaondoa Bi Mboko na Bw Mbogo.

Mwenyekiti wa vuguvugu hilo, Bw Salim Karama, alisema wabunge hao wawili wameonyesha hawajali maslahi ya wakazi waliowachagua kuhusiana na ubebaji mizigo kupitia SGR.

Hatua yao ilijiri huku Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi akiikataa hoja ya Bw Ali kwa madai haikuwa na ushahidi.

Bw Ali alikuwa akitaka Bunge lipitishe hoja ya kutokuwa na imani na Bw Macharia, anayedai amedharau mahakama na katiba kuhusu kuwashirikisha wakazi wa Pwani kabla ya kuhamisha mizigo kutoka Mombasa hadi Nairobi na Naivasha.

Jumanne, Bw Ali aliapa kuendeleza juhudi za kusukuma hoja hiyo: “Kuna watu waliokuwa wanasema hoja yangu itakufa tu hapo kwa Spika kwani kuna maagizo kutoka juu. Leo nitamwandikia barua niweke huo ushahidi anaotaka na nimpatie. Kawaida ukienda mahakamani, unatoa ushahidi ukiwa hapo,” akasema Bw Ali.

Alitaka kujua ni kwa nini hoja yake ilipitishwa katika afisi ya Katibu wa Bunge kama kweli haikuwa imezingatia kanuni zote.

“Hii ni njama tu. Kwa nini hoja zote zilikubaliwa hadi leo ndipo niambiwe kwamba sijatimiza jambo fulani? Nitafuatilia hoja yangu hadi mwisho. Na iwapo majaribio yote yatashindwa, basi nitarejea kwa watu wa Pwani watoe mwelekeo,” akasema.

WAKAZI WASIKATE TAMAA

Mbunge wa Mvita Bw Abdulswamad Nassir alisema wakazi wa Pwani hawapaswi kukata tamaa, kwa kuwa bado kuna mswada wake unaotaka kusimamishwa kwa utumizi wa SGR kupeleka mizigo ya watu wa Mombasa hadi Naivasha.

“Mswada wangu bado upo bungeni. Tulitaka ufafanuzi kuhusu masuala kadhaa. Sikuunga mkono ule wa Mohaa kwa sababu sikutaka nionekane sina msimamo. Huu wangu unakwenda sambamba na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuwa kutumia SGR kubeba mizigo kunaathiri uchumi wa Pwani,” akasema Bw Nassir.

Bi Mboko alisema hakuunga hoja ya Bw Ali kwa kuwa amekuwa akijifanyia mambo kivyake ‘bila kutafuta ushauri’.

Serikali imesababisha wakazi wengi wa Pwani kupoteza kazi na biashara kwa kuagiza kontena zote zisafirishwe kwa reli ya SGR, wanaoumia zaidi wakiwa madereva wa matrela pamoja na wanaotoa huduma barabarani kama za mikahawa na malazi.

Masaibu ya Wapwani yameongezeka zaidi baada ya serikali kuagiza mizigo iwe ikishughulikiwa jijini Nairobi badala ya Mombasa, hatua ambayo imewanyima makuli na wenye mabohari ya mizigo kazi.

Wiki iliyopita, mahakama ilisimamisha agizo lingine la Serikali kuwa mizigo inayoenda Uganda na mataifa mengine jirani ipelekwe hadi Naivasha kwa SGR.