Kimataifa

Bangi aliyovuta Bob Marley ni safi kuliko ya sasa – Msomi

June 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MTAFITI hatimaye amegundua bangi ya asili iliyokuwa ikivutwa na mwanamuziki nguli wa reggae Bob Marley kati ya miaka ya 1950s na 1970s.

Dkt Machel Emanuel ambaye ni mhadhiri katika kitivo cha Biolojia katika Chuo Kikuu cha West Indies, Kingston, anasema wasanii wa kundi la muziki wa regaee, The Wailers, walitumia bangi tofauti na ile inayovutwa sasa.

Kulingana na Dkt Emanuel, Bob Marley, Peter Tosh na Bunny Wailers ambao ni waasisi wa kundi la The Wailers, walitumia bangi ya asili iliyokuwa na makali ya kadri tofauti na ya sasa inayofanya watumiaji kuchanganyikiwa au kurukwa na akili.

Mtafiti huyo aliye na bustani kubwa ya bangi chuoni West Indies anasema kuwa bangi ya asili iliyokuwa ikitumiwa na akina Bob Marley ilikuwa ikimea yenyewe bila kupandwa.

Anasema bangi inayotumiwa sasa mbegu zake zimechanganywa makali ya THC ambayo husababisha watumiaji wake kulewa haraka na hata kuharibu akili zao.

“Katika ya 1950, 1960 na 1970, Jamaica ilikuwa na bangi tamu kupindukia iliyoizolea Jamaica sifa tele kimataifa,” akasema msomi huyo ambaye rastafari.

Anasema bangi waliyovuta akina Bob Marley ina maua na harufu tofauti na bangi inayovutwa sasa.

Kulingana na msomi huyo, bangi hiyo ya asilia iling’olewa miaka ya 1980 wakati Amerika ilikuwa ikiendesha operesheni dhidi ya dawa za kulevya.

“Miti ya bangi hii asilia ni mirefu na maua yake yanaonekana kutoka mbali. Hivyo ilikuwa rais kwa serikali kuing’oa na kuimaliza. Miaka michache baadaye, bangi asilia iliisha na watu kuanza kupanda mbegu za kisasa,” akaelezea Dkt Emanuel, 35.

Msomi huyo havuti moshi wa bangi lakini huitumia kwa njia ya mvuke.

Mtafiti huyo alipata mbegu za bangi ya asili na kuzizalisha kisayansi katika maabara yake. Ndani ya maabara hiyo picha kubwa ya aliyekuwa kiongozi wa Ethiopia Haile Selassie anayechukuliwa kuwa Masia wa Warastafari, inaning’inia ukutani.

Anasema kuwa alifanikiwa kupata mbegu za bangi hiyo asilia kutoka kwa mtu ambaye amekuwa akiishi milimani peke yake.

“Mtu huyo amekuwa akiishi peke yake na amejitenga na watu kwa miaka mingi. Anaishi maisha ya upweke. Hapo ndipo nilipata mbegu za bangi ya kiasili,” akasema.

Mwanasayansi huyo anasema kuwa bangi hiyo ya asili huenda ikawa kipenzi cha wengi hivyo kuieleta Jamaica mapato makubwa.

Jamaica ni miongoni mwa nchi ambazo bangi imehalalishwa na huvutwa hadharani.