Habari Mseto

Bangi iliyofichwa kama peremende yanaswa JKIA

August 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MAMLAKA ya Kukusanya Ushuru (KRA) Jumatano ilikamata dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Dawa hizo zilikuwa zimefichwa kama tembe za vitamini ambazo zilikuwa zimewekwa ndani ya vibweta 26 ambavyo vilikuwa vimetiwa mafuta yaliyotengenezwa kutokana na bangi.

Pia walipata pakiti tano, kila moja iliyokuwa na gramu moja ya bangi.

“Dawa hizo zilikuwa zimetumwa kupitia kwa huduma ya uchukuzi na zilikuwa zimetangazwa kama peremende,” alisema kamishna wa forodhani na usimamizi wa mipaka wa KRA Julius Musyoki katika taarifa.

Dawa hizo zilikamatwa na maafisa wa forodhani wa KRA wakati wa shughuli za kawaida katika eneo la mizigo.

Kifurushi hicho kilikaguliwa na baada ya ukaguzi wa kina, ilibainika kuwa zilikuwa ni dawa za kulevya.

Hatua hiyo ni katika juhudi za kumaliza dawa za kulevya nchini na mashirika husika.