Habari Mseto

Bangi iliyosafirishwa kwa lori la mafuta yanaswa

May 20th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

POLISI Kaunti ya Nakuru Jumatatu walinasa bangi ya dhamana ya Sh3.6 milioni, ambayo ilikuwa ikisafirishwa katika lori la kusafirisha mafuta.

Maafisa hao ambao walikuwa wametoka Jijini Nairobi baada ya kupata habari kuhusu gari hilo waliliandama kwa zaidi ya kilomita 100, kabla ya kulinasa na kumtia nguvuni dereva wake.

Gari hilo liliripotiwa kuwa lilikuwa likitoka eneo la Wajir na kuwa lilikuwa likisafirisha mihadarati hiyo kuelekea pahali pasipojulikana, likishukiwa kuwa lilitoka taifa jirani.

“Leo maafisa wa kitengo spesheli cha kupambana na uhalifu kutoka Nairobi walipata habari kuwa lori la mafuta lilikuwa likisafirisha mihadarati kutoka Wajir kuelekea mahali pasipojulikana.

“Maafisa hao walianza kuliandama gari hilo lakini wakalipoteza walipofika Thika, hata hivyo, baadaye walilipata likiwa limeegeshwa Nakuru, ambapo walilikamata,” akasema Kamanda wa polisi Kaunti ya Nakuru Stephen Matu.

Maafisa hao walipata gari hilo likiwa limeegeshwa eneo la Mwariki, viungani mwa mji huo, ambapo walimkamata dereva.

“Walimkamata dereva ambaye walimpata katika gari hilo na wakampeleka katika kituo cha polisi cha Nakuru Central. Tulikata tanki hilo kwa kuwa mihadarati ilikuwa imejazwa ndani na tukapata mihadarati inayoshukiwa kuwa bangi ya dhamana ya takriban Sh3.6 milioni,” akasema Bw Matu.

Alisema kuwa polisi wanaendelea kuwinda washukiwa wengine, akisema dereva wa gari hilo atafikishwa kortini Jumanne.

Polisi walisema hiyo ndiyo mihadarati ya kiwango kikubwa sana kuwahi kukamatwa kaunti hiyo.

“Hapa Nakuru hatujawahi kukamata mihadarati mingi kiasi hiki, lakini tunashuku ilitoka katika taifa jirani eneo la kaskazini mwa Kenya,” akasema kamanda huyo.