Habari Mseto

Bangi ni hatari kwa akili za watoto – Utafiti

October 5th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

VIJANA wa umri mdogo ambao wanatumia bangi wanajisababishia matatizo ya muda mrefu katika akili zao ambazo ziko katika hali ya kukua. Hii ni kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi moja nchini Canada.

Utafiti huo ulionyesha kuwa bangi huathiri namna ya kufikiria, kumbukumbu za akili na tabia kuwa mbovu, ikilinganishwa na za vijana wanaotumia pombe.

Watafiti hao kutoka chuo kikuu cha Montreal wameshauri vijana kutoanza kutumia bangi wakiwa wachanga, wakiwarai kuvumilia kwa hali na mali hadi wafikapo umri mkubwa.

Hii ilikuwa baada ya kuwapima vijana 3,800 katika kipindi cha miaka minne, wakiwa wa umri wa kuanzia miaka 13.

Unywaji wa pombe na kuvuta bangi mtu akiwa wa umri mdogo husababisha matatizo ya kiakili na kuathiri mambo kama elimu, umakinifu wa mawazo na namna ya kufanya maamuzi ya kimaisha.

Utafiti huo ulibaini kuwa matatizo hayo yalizidi kuongezeka miongoni mwa vijana, kadri matumizi ya bangi yalivyopanda, huku matatizo hayo yakiwa ya muda mrefu, ikilinganishwa na vijana waliotumia pombe.

Vijana hao kutoka shule 31 tofauti za huko Canada walitoa habari kuhusu hulka zao za kutumia dawa za kulevya na pombe mara moja kila mwaka.

Akili zao aidha zilipimwa kila mwaka shuleni, kupitia mtambo wa kikompyuta wa kupima akili za mtu.

Ingawa kiwango cha matumizi ya bangi katika utafiti huo kilikuwa chini ikilinganishwa na matumizi ya pombe, asilimia 28 ya vijana walikiri kuwahi kuitumia.

Asilimia 75 ya vijana nao walikiri kuwa wametumia pombe nyakati fulani.

Profesa Patricia J Conrod ambaye ndiye mtafiti mkuu kutoka idara ya masomo ya akili chuo cha Montreal alisema alitarajia kuwa ni pombe ambayo ingekua imewaadhiri vijana zaidi lakini ikawa bangi.