Kimataifa

Bangladesh sasa chini ya wanajeshi baada ya Gen Z kutimua Waziri Mkuu


DHAKA, Bangladesh

MKUU wa Majeshi Bangladesh Waker-Uz-Zaman ametangaza mipango ya kuundwa kwa serikali ya muda nchini humo, uongozi sasa ukiwa chini ya utawala wa jeshi.

Jenerali Zaman alitoa tangazo hilo Jumatatu, Agosti 5, 2024 muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Sheikh Hasina kujiuzulu kutokana na uasi wa raia dhidi ya utawala wake.

Mkuu huyo wa majeshi alihimiza raia kudumisha utulivu na kukomesha maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Jenerali Zaman vile vile alirai raia wa nchi hiyo kuwa na imani kuwa wanajeshi watasaidia katika kurejeshwa kwa uthabiti nchini humo.

“Tumewaalika wawakilishi kutoka kwa vyama vyote vikuu vya kisiasa, na wamekubali mwaliko wetu na kutoa hakikisho kuwa watashirikiana nasi,” akaeleza.

Mkuu huyo wa majeshi aliahidi kuwa wale waliotekeleza udhalimu dhidi ya waandamanaji wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Vile vile, tutahakikisha kuwa haki imepatikana kwa vifo vyote na uhalifu uliotokea wakati wa maandamano,” akaongeza.

Sheikh Hasina, 76, na dadake, Sheikh Rehana walioondoka jijini Dhaka Jumatatu asubuhi (Agosti 5, 2024) wakitumia helikopta.

Vyombo vya habari nchini Bangladeshi viliripoti kuwa walielekea India.

Awali, waandamaji waliingia katika makazi ya Waziri Mkuu huyo yaliyoko katika jumba la Ganobhaban.

Zaidi ya watu 300 wamekufa na maelfu kujeruhiwa katika machafuko yaliyoanza kushuhudiwa nchini humo katikati mwa Julai 2024, wanafunzi wa vyuo vikuu wakipinga mfumo wa ugavi wa nafasi za ajira katika utumishi wa umma.

Jumapili, Agosti 4, 2024 pekee watu 98 waliuawa katika makabiliano makali jijini Dhaka na maeneo ya karibu.