Michezo

Bao la Martial kwa Melanie lahesabiwa rasmi na refa wa mahaba

July 30th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Manchester United, Anthony Martial ameingia katika orodha ya vidume kamili baada ya bao alilomfunga kipusa Melanie Da Cruz mnamo Oktoba 2017 kuhesabiwa rasmi na refa wa mahaba.

Baada ya kuarifiwa kuhusu hali ya mchumba wake, Martial alilazimika kuondoka ghafla kambini mwa Man-United nchini Amerika na kutua jijini Paris, Ufaransa kushuhudia kuzaliwa kwa kimalaika Swan.

Ujio wa Swan kwa sasa kunamfanya Martial, 22, kuwa baba wa watoto wawili.

Kabla ya kuanza kujirinia asali mzingani mwa Melanie mnamo 2016, Martial alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na kichuna Samantha Jacquelinet aliyemzalia mtoto wa kike, Peyton mwenye umri wa miaka miwili.

Akipania kutangazia ulimwengu mzima ukubwa wa furaha yake, Martial alitumia mtandao wa Instagram kupakia picha iliyoonesha sehemu za miguu ya mtoto Swan na kuambatanisha maelezo: “Mungu nakushukuru kwa kunipa mtoto wa pili ambaye amezaliwa leo akiwa mwingi wa afya.”

Kwa upande wake, Melanie ambaye ni mwanahabari maarufu nchini Ufaransa, alipakia mtandaoni picha zake za awali na kuandika, “Nawashukuru nyote. Jina ni Swan Anthony Martial. Mungu akubariki mwanangu.”

Akihojiwa na gazeti la The Sun mwishoni mwa mwezi jana, Samantha alikiri kwamba kusambaratika kwa ndoa kati yake na Martial kulichangiwa na mwanamuziki Emily Wademan aliyeanza kumwanikia mwanasoka huyo tunda lake mwanzoni mwa 2016.

Baada ya jaribio la Samantha kurudiana na Martial kugonga mwamba, kidosho huyo alianza kumpaka tope Melanie kwa kudai kuwa alikuwa kahaba aliyewania penzi la aliyekuwa mumewe kwa nia ya kuzifakamia hela zote za mchezaji huyu.

Isitoshe, Samantha alidai kuelewa urefu wa historia ya Melanie katika kuwalaghai wanaume na kuzinyonya hela zao na hivyo kumtaka Martial ajiandae kutemwa pindi ‘chemchemi yake ya fedha itakapokauka’.

Hadi kufikia mwisho wa mwaka jana, Samantha alikuwa akiteswa na uhalisia wa kuyakosa mapenzi motomoto ya Martial ambaye alipania kuponda raha ya ujana na Melanie nchini Mauritius baada ya kocha Didier Deschamps kutomteua kuunga kikosi kilichonyanyulia Ufaransa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka huu.

Baada ya uhusiano wa Martial na kocha Jose Mourinho kudorora, huduma za fowadi huyu zinawaniwa kwa sasa na Juventus, Borussia Dortmund, Chelsea na Tottenham Hotspur.