DOUGLAS MUTUA: Bara Afrika linaonewa kwa kugundua kirusi ‘omicron’

DOUGLAS MUTUA: Bara Afrika linaonewa kwa kugundua kirusi ‘omicron’

Na DOUGLAS MUTUA

MATAIFA ya Afrika yamekuja juu baada ya yale ya Magharibi kupiga marufuku wasafiri wanaotokea Afrika kwa hofu kwamba wataeneza aina mpya ya virusi vya korona.

Ama kweli, aina hiyo mpya inayojulikana kama ‘omicron’ imewapa wengi hofu kwa kuwa hata wanasayansi hawana hakika iwapo inazimwa na chanzo za korona zilizopo au la.

Si hayo tu! Hata kabla ya omicron kutangazwa Afrika Kusini kwa mara ya kwanza, maambukizi ya korona katika mataifa ya Magharibi yalikuwa yamekwisha anza kupanda tena.

Kisa na maana msimu wa baridi umeingia na kutokana na hali ilivyokuwa mwaka jana, inakisiwa kuwa mazingira ya baridi huwezesha ugonjwa huo kuenea kwa kasi.

Hivyo basi, kuzuka kwa omicron lazima kumeleta hofu maradufu kwa mataifa ambayo hupata msimu wa baridi ya mzizimo kila mwaka.

Hawajui waanzie wapi; wakabili maambukizi ya awali au washughulikie virusi hivi vipya ambavyo vinatishia kuangamiza wengi.

Tangazo la Marekani, Uingereza na mataifa mengine kwamba wasafiri wanaotokea eneo la kusini mwa Afrika wamepigwa marufuku limepokelewa kwa hasira zaidi na Afrika Kusini.

Rais Cyril Ramaphosa amesema hiyo ni hatua ya kibaguzi isiyofaa hata kidogo kwa kuwa itayaathiri vibaya mataifa yanayolengwa.

Amekariri kuwa inasikitisha kuona mataifa hayo yakiadhibiwa kwa kuwa wanasayansi waliomo wametenda wema kwa kuifahamisha dunia ipo hatari mpya.

Bw Ramaphosa ameteta kuwa yalikoanzia maradhi ya korona kunajulikana wala hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yako.

Labda ni kutokana na nguvu ilizonazo Uchina?

Binafsi nina hakika kuwa marufuku hii ni ya muda tu na inanuiwa kuwapa wanasayansi wa mataifa ya Magharibi muda wa kutosha kuielewa omicron na kutoa mwelekeo.

Vilevile, nadhani serikali za Magharibi zimo mbioni ama kutengeneza chanjo mpya au kuboresha zilizopo ili kukabili omicron na aina nyinginezo zilizozuka.

Kwa taarifa yako, kufikia sasa kuna aina 50 za virusi vya korona.

Kinachosababisha niamini kuna jambo la kutia hofu ambalo wanasayansi wameona katika omicron ni kwamba aina nyingine hazijazua hofu kiasi hicho.

Virusi aina ya ‘delta’ ndivyo vilivyohangaisha sana, lakini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa baada ya wanasayansi kugundua kwamba chanjo zilizopo zinavidhibiti kwa asilimia kubwa.

Huku tukisubiri wanasayansi watwambie kuhusu hatari ya omicron, ni sharti kila mtu awajibikie afya yake binafsi.

Kufikia sasa nadhani aliye na akili razini amefunzwa na korona jinsi maisha yalivyo binafsi; anayeaga dunia anazikwa na kusahaulika ghafla, watu wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

Labda ni kwa kuwa vifo vimekuwa vingi tu tangu mwaka 2020? Huenda ikawa, na ndiyo sababu nasisitiza mtu binafsi ajijali zaidi.

Aliye na maradhi yanayopunguza kinga mwilini mwake hapaswi kushuritishwa kuchukua hatua za kujiweka salama.

Uzembe na kutojali utamsukuma kaburini ghafla!

Kufikia sasa, hali ilivyo kwenye mataifa ambayo yana chanjo za kutosha inatusadikisha kuwa janga la korona limesalia kuwa la watu wasiochanjwa.

Asilimia zaidi ya 90 ya watu wanaougua na kulazwa hospitalini ni waliokataa chanjo, hivyo hatari ya kufariki kutokana na ugonjwa huo ipo katika kususia chanjo.

Nchini Kenya na Afrika kwa jumla, ambako waliochanjwa ni wachache mno, hatua za kimsingi za kujikinga kama vile kuvaa barakoa na kutokwenda kuliko na watu wengi zitafaa sana.

Kunawa mikono vilevile.

Raia wakichukua hatua madhubuti, hakutakuwa na sababu za serikali kufunga chumi za dunia, hatua ambayo imetokea kuumiza watu kuliko korona yenyewe.

Nchini Kenya, ambako wizi wa mali ya umma ni uraibu na mazoea, mara hii wezi wabanwe na kusombwa mbali na mfuko wa korona ili tusirudie laana tulizokariri tayari.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Shujaa yanyoa Amerika ya kocha Mike Friday bila maji raga...

Kocha wa Senegal amtaka Klopp aheshimu AFCON

T L