Habari Mseto

Barabara ya umbali wa kilomita 75 ya Gatundu-Juja Farm kujengwa

November 5th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Juja Farm na maeneo ya karibu watatabasamu wakati barabara ya lami itakapojengwa kuwafaa jinsi ambavyo mikakati imewekwa.

Katibu katika Wizara ya Uchukuzi Bw Paul Maringa akiwa eneo la Juja alisema Jumanne barabara ya umbali wa kilomita 75 kutoka Gatundu hadi Juja Farm tayari imezinduliwa ambapo wahandisi wa kampuni ya H-Young wako mashinani.

Alisema barabara hiyo itagharimu takribani Sh3.9 bilioni na inaendelea kwa mfululizo bila shughuli hiyo kusitishwa.

“Tunaelewa vyema biashara nyingi zitanawiri wakati mradi huo utakapokamilika. Kwa hivyo tunataka wakazi wa maeneo hayo wadumishe ushirikiano mwema baina yao na wahandisi hao,” alisema Bw Maringa.

Alisema barabara ya umbali wa kilomita 35 kuelekea Gatuanyaga pia itaunganishwa na hiyo ya Gatundu.

Alifafanua kwamba barabara hiyo inajengwa na Halmashauri ya Ujenzi wa Barabara za Mashinani (KeRRA).

Inatarajiwa kuwa ya kiwango cha kisasa ambapo itapanuliwa iwe kubwa ili magari makubwa yaweze kupita hapo.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, ambaye pia aliandamana na katibu huyo alipongeza serikali kwa kuwajali wakazi wa Juja Farm ambao kwa muda mrefu wamekuwa na shida ya usafiri.

Nyoro alisema baada ya barabara hiyo kukamilika umeme utasambazwa ili kurahisisha biashara na kupunguza uhalifu.

Aliwajulisha wakazi wa Juja kuwa iwapo wanataka maslahi yao yazingatiwe vilivyo ni lazima waachane na siasa za kila mara zisizo na maana.

“Kwa wakati huu tumesalia na miaka miwili pekee na kwa hivyo ni vyema kujiepusha na siasa za mapema,” alisema Bw Nyoro.

Aliwahimiza wahandisi wanaoendesha mradi huo kuhakikisha vijana walio katika maeneo hayo wanapewa nafasi ya kwanza kupata ajira.

“Halitakuwa jambo la busara iwapo watu wa kutoka maeneo mengine ndio watapewa nafasi huku vijana wetu wakiachwa hoi,” alisema Bw Nyoro.

Alisema Kaunti ya Kiambu itakuwa mstari wa mbele kufuatilia ukarabati wa barabara hiyo.

Aliwataka maafisa wote wanaofanya kazi katika kaunti hiyo kuwa mstari wa mbele kuchapa kazi bila kuchambana wala kufarakana.

Alisema kila afisa ana wajibu wake aliopewa kufanya na kwa hivyo hiyo ni muhimu ili kuinua kaunti nzima ya Kiambu.