Habari Mseto

Baadhi ya barabara za jiji la Nairobi kufungwa Jumapili

October 26th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

USAFIRI utavurugwa Jumapili katikati mwa jiji la Nairobi kwani baadhi ya barabara zenye shughuli nyingi zitafungwa ili zitumike mahususi kwa mbio za Marathon za kila mwaka za Standard Chartered.

Kamanda wa Trafiki katika Kaunti ya Nairobi Joshua Omukata, kwenye taarifa Jumamosi, amesema barabara zitakazofungwa ni pamoja na; Lower Hill Road, Museum Hill, Forest Road, University Way na Langata Road.

“Katika eneo la katikati mwa jiji, barabara ya Kenyatta Avenue, sehemu za Haile Selassie Avenue na Harambee Avenue pia zitaathirika,” imesema taarifa hiyo.

Barabara hizo zitafungwa kuanzia Jumamosi saa tano za usiku hadi Jumapili saa nane alasiri.

Bw Omukata amewahakikishia wenye magari kuwa kutakuwa na maafisa wa kutosha kuyaelekeza magari katika makutano mbalimbali ya barabara.

Magari ambayo yatakuwa yakielekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumapili yatalazimika kufanya mipango ya mapema kusafiri ili kuzuia usumbufu.

Zaidi ya watu 30,000 watashiriki katika mbizo hizo zinazolenga kukusanya Sh60 miliomi kufadhili mpango wa kuwasaidia vijana unaojulikana kama; “Future Makers”.

Mbio hizo za marathon zitaanza asubuhi katika barabara ya Uhuru Highway, karibu na Uwanja wa Nyayo na watatumia mzunguko wa barabara ya Bunyala kuelekea Mombasa Road, kupitia barabara ya Forest Road na kisha warejeee tena Uwanja wa Nyayo.