Barasa aamrisha idara ya afya idhibiti ebola

Barasa aamrisha idara ya afya idhibiti ebola

Kakamega inapakana na Kaunti ya Busia ambayo ipo mpaka wa Kenya na Uganda.

Tayari ebola imeripotiwa kusababisha vifo Uganda japo raia wa nchi hizo mbili bado wanatangamana kupitia mji wa mpaka wa Malaba.

Wiki jana, Ebola iliripotiwa kusababisha vifo vya watu saba Uganda huku wagonjwa wengine wakiendelea kulazwa katika hospitali mbalimbali wakipokea matibabu.

Bw Barasa alisema wafanyabiashara wengi kutoka Kakamega hupokea bidhaa zao kutoka Uganda kupitia Busia.

Alidai kuwa iwapo ukaguzi hautafanywa basi Kakamega ni kati ya kaunti ambazo ebola inaweza kufika.

“Namwaamrisha waziri wa afya aweke mikakati ya kiafya ambayo itawalinda watu wetu dhidi ya virusi vya ebola. Pia nawaomba wakazi wa Kakamega wajihadhari wanapoendelea na majukumu yao kuzuia ebola,” akasema Bw Barasa.

Gavana huyo alikuwa akizungumza katika hafla ya kusherehekea ushindi wa diwani wa wadi ya Marama ya Kati Philip Maina.

Bw Barasa pia aliahidi kuwa utawala wake utatoa mafunzo na kushiriki mahamasisho kwa raia ili wafahamu jinsi ya kukabiliana na kudhibiti ebola.

“Nawaomba raia wetu wapige ripoti iwapo wanashuku kuwa yeyote anaugua ebola. Wafahamishe wahudumu wetu wa kiafya pamoja na idara za kiusalama,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) dalili za anayeugua ebola huanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21.

Zaidi ya asilimia 90 ya watu ambao wana ebola hufa haraka.

Kati ya dalili zake ni maji kutoka mwilini, kijibaridi, kutapika, kutokwa damu na kuendesha.

Kuchipuka kwake ni vigumu kudhibiti hasa katika maeneo ya mabanda ambako kuna watu wengi.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mwezi huu Septemba alitoa tahadhari kufuatia kuchipuka kwa ebola Uganda na kuwataka maafisa wa afya na wale wa usalama wawe chonjo mpakani.

Hata hivyo, kufikia Jumapili, ukaguzi au vipimo vya kimatibabu havikuwa vimeanza Busia na Malaba huku raia wa Uganda wakiingia na kutoka nchini bila kufanyiwa vipimo vya kiafya.

  • Tags

You can share this post!

Wazee Mlimani waapa kuleta Kenya pamoja

Mkenya Karan Patel aibuka mshindi wa Rwanda Mountain...

T L