Barasa kortini kudai fidia baada ya IEBC kuahirisha uchaguzi

Barasa kortini kudai fidia baada ya IEBC kuahirisha uchaguzi

Bw Barasa, ambaye ndiye mwaniaji ugavana wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, aliilaumu tume hiyo kwa kutojali.

Vile vile, aliilaumu Idara ya uagizaji katika tume hiyo kwa kukosa kuzingatia taratibu zifaazo kwenye ununuzi wa vifaa vya uchaguzi.

“Kundi la makamishna lilisafiri hadi nchini Ugiriki kukagua na kufuatilia uchapishaji wa karatasi za uchaguzi. Wakati waliporejea, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, aliwahakikishia Wakenya kwamba kila kitu ki shwari. Ninahisi kuna njama fiche baada ya tume kusimamisha uchaguzi kwa kisingizio kuwa kulikuwa na kosa kwenye uchapishaji wa karatasi hizo,” akasema Bw Barasa.

Bw Barasa, ambaye alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kusambaza Umeme (Ketraco), alisema tayari amewaagiza mawakili wake kuishtaki tume kwa hasara aliyopata.

Alisema alitumia fedha nyingi wakati wa kampeni.

“Lazima niishtaki IEBC kwa hasara niliyopata. Sababu kuu ni kuwa itanigharimu pesa kujiandaa tena kwa uchaguzi huo. Matayarisho hayo yatahusu kuwalipa maajenti kati ya masuala mengine. Tulikuwa tayari tushawalipa maajenti na kuwatuma katika vituo tofauti vya kupigia kura hadi pale tume ilitangaza imeahirisha uchaguzi. Lazima inilipe fidia kwa hasara niliyopata,” akasema.

Bw Barasa pia anaitaka tume kukagua tena Mitambo ya Kusimamia Uchaguzi (KIEMS) ili kuhakikisha inaepuka hali ambapo mitambo hiyo inakosa kufanya kazi uchaguzi unapowadia.

Alisema mitambo hiyo ilikosa kuwatambua wapigakura wengi wakati wa uchaguzi.

“IEBC inafaa kutathmini kwa kina mitambo yake ili kuhakikisha mitambo inayotumika imo katika hali nzuri,” akasema.

Awali, muungano huo ulikuwa umeeleza tashwishi kuhusu hatua ya tume kuahirisha uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Kakamega na Mombasa.

Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega, alidai kwamba makosa hayo ya uchapishaji yalitokea tu kwenye maeneo ambako ni ngome za mwaniaji urais wa Azimio, Bw Raila Odinga.

“Yeyote ambaye atapatikana kuhusika kwa vyovyote katika kosa hilo anafaa kuadhibiwa kulingana na Sehemu 6 (J) ya Sheria za Uchaguzi,” akasema Bw Oparanya.

Kando na kaunti za Kakamega na Mombasa, sehemu nyingine zilizoathiriwa na tatizo hilo ni maeneobunge ya Kacheliba na Pokot Kusini.

Baadhi ya makosa yaliyoonekana kwenye karatasi za uchaguzi za maeneo hayo ni uwepo wa picha zisizofaa na maelezo ya wawaniaji.

Karatasi za uchaguzi za Kaunti ya Kakamega zilikuwa na maelezo ya wawaniaji waliowania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga.

Watu saba wamejitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwemo Seneta Cleophas Malala.

  • Tags

You can share this post!

Changamoto kwa Sakaja huku muungano wa Azimio ukitawala jiji

Nguvu za Ruto Mlimani zatikisa usemi wa Rais

T L