Habari za Kitaifa

Baraza la Mawaziri launga vita dhidi ya vileo haramu

March 14th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

BARAZA la Mawaziri limeunga mkono kikamilifu juhudi za Wizara ya Usalama wa Ndani kukabiliana na kero ya pombe haramu na mihadarati nchini.

Hatua hizo zilizotangazwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki zinajumuisha kusitishwa kwa leseni za kampuni 52 za kutengeneza pombe ya daraja la pili ambayo huwa ya bei nafuu kiasi na kufutiliwa mbali kwa leseni zote zilizotolewa kwa baa na serikali za kaunti kinyume cha sheria.

Pia aliagiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa usalama wanaoendeleza matumizi ya vileo hivyo.

Hatua nyingine ni kama vile operesheni kote nchini dhidi ya uuzaji na matumizi ya pombe haramu.

“Afisa yeyote wa umma anayehujumu hatua za kupambana na pombe haramu na mihadarati atakuwa anakwenda kinyume na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba na sheria husika. Afisa kama huyo atachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria,” ikasema taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Nairobi.

Mkutano huo uliongozwa na Rais William Ruto.

Miongoni mwa maafisa walioonywa dhidi ya kuhujumu vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati ni maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Maafisa wa Utawala wa Kimkoa, Maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini, Maafisa wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs), Maafisa wa Afya ya Umma na Maafisa wa Ofisi ya Mwendesha Mshtaka Mkuu, miongoni mwa wengine.

Mkutano huo ulielezwa kwamba tangu Wizara ya Usalama wa Ndani ilipoanza kutekeleza hatua hizo, vituo 2,393 vya kuuza pombe vimefungwa sawa na maduka 359 ya kuuza dawa na mengine 452 ya kuuza dawa za kutumika katika shughuli za kilimo (agrovet).

“Aidha, maafisa wa usalama wametekeleza mavamizi 5,835 katika vituo vya kuuza pombe haramu na dawa za kulevya huku lita 289,390 za pombe haramu na lita 13,198 za pombe ghushi zikinaswa,” taarifa hiyo ikasema.

Aidha, magari saba ya kusafirisha dawa za kulevya, misokoto 3,603 ya bangi na marobota 44 yalinaswa.

“Kufuatia ongezeko la matumizi ya pombe na mihadarati, Baraza la Mawaziri liliamuru Wizara ya Afya kuandaa mwongozo wa ujenzi wa wodi maalum za kuwatibu waathiriwa katika hospitali zote za kiwango cha Level 5,” ikasema taarifa hiyo.

Wizara hiyo pia iliagizwa kushirikiana kwa karibu na serikali za kaunti kuhakikisha kuwa vituo hivyo vya kuwatibu waraibu wa pombe na mihadarati vinafanya kazi.