Kimataifa

Baraza tawala lavunja chama cha Bashir, kunadi mali yake

November 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

WATAWALA wapya nchini Sudan, Alhamisi waliagiza chama cha Rais aliyetimuliwa mamlakani Omar al-Bashir, kivunjwe na utawala wake kusambaratishwa, walivyotaka waandamanaji ambao waliendesha kampeni ya kumuondoa mamlakani.

Bashir chini ya chama chake cha Islamist National Congress Party (NCP), alikuwa ametawala nchi hiyo ya Afrika Kaskazini tangu 1989 kabla ya kubanduliwa mamlakani kupitia maandamano ya kitaifa mapema mwaka huu.

Baraza jipya linalotawala nchi hiyo na baraza lake la mawaziri linaloongozwa na waziri mkuu Abdalla Hamdok liliamua chama hicho kivunjwe, kwa kuidhinisha sheria inayofahamika kama “ kuvunjwa kwa utawala ya Juni 30, 1989”.

“Chama cha The National Congress Party kimevunjwa na usajili wake umefutwa kutoka orodha ya vyama vya kisiasa nchini Sudan,” lilisema agizo la baraza tawala na kuongeza kuwa kamati itaundwa itakayotwaa mali yote ya chama hicho.

“Hakuna alama yoyote ya chama itakayoruhusiwa kushiriki katika vitendo vya kisiasa kwa miaka kumi,” iliongeza.

Waziri Mkuu Hamdok alisema kupitia Twitter kwamba, kuvunjwa kwa chama hicho sio kulipiza kisasi dhidi ya watawala wa zamani wa nchi hiyo.

“Lakini lengo ni kulinda heshima ya watu wa Sudan ambayo walinyimwa na watu wasio waaminifu. Sheria hii inalenga kukomboa utajiri wa watu ulioporwa,” msemaji wa vuguvugu la Forces of Freedom and Change, Wajdi Salah, aliandika katika ukurasa wake wa Facebook.

Chama cha Wataalamu wa Sudan (SPA), kilichokuwa cha kwanza kuongoza maandamano dhidi ya Bashir, kilipongeza kuvunjwa kwa utawala wa zamani.

“Ni hatua muhimu kuelekea kuafikia lengo la wanamageuzi la kujenga taifa la demokrasia,” SPA ilisema kupitia taarifa.

Waandamana

Maelfu ya raia wa Sudan walikusanyika Oktoba 2019 katika miji kadhaa ya nchi hiyo wakitaka chama hicho kuvunjwa.

Bashir alitumia chama hicho kutawala Sudan kimabavu tangu 1989 alipotwaa mamlaka kwa kupindua serikali ya kiraia ya waziri mkuu Sadiq al-Mahdi.

Mnamo Alhamisi, baraza kuu tawala na baraza la mawaziri zilifutilia mbali sheria iliyonyima wanawake haki zao katika nchi hiyo chini ya utawala wa Bashir.

Maelfu ya wanawake walicharazwa mijeledi, kutozwa faini na kufungwa jela chini ya sheria hiyo ya Kiislamu.

Sheria hiyo iliwakera wanawake kwa miongo mingi na walikuwa msitari wa mbele kwenye maandamano yaliyolipuka Desemba 2018 dhidi ya Bashir. Aliondolewa mamlakani na jeshi Aprili 11 na mnamo Agosti, jeshi na raia waliunda baraza tawala kusimamia kipindi cha mpito walivyotaka waandamanaji.

Bashir anazuiliwa katika gereza moja jijini Khartoum akikabiliwa na mashtaka ya ufisadi.