Michezo

BARCA NI BAADAYE: Neymar haingii Camp Nou hivi karibuni

August 6th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

NAIBU Rais wa Barcelona, Jordi Cardoner amefutilia mbali uwezekano wa miamba hao wa soka ya Uhispania kumsajili upya mvamizi Neymar Jr msimu huu.

Yamekuwa matamanio makubwa ya Neymar kubanduka kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) muhula huu na kurejea Barcelona walioagana naye miaka miwili iliyopita kwa kima cha Sh26 bilioni.

Licha ya presha kutoka kwa Real Madrid, Barcelona wanapigiwa upatu kujinasia huduma za Neymar, 27, na tayari wamefichua azma ya kumshawishi kujiunga nao kwa mkopo kabla ya kumpa mkataba wa kudumu mwishoni mwa msimu huu.

Kulingana na Cardoner, njia ya pekee kwa Barcelona kwa sasa kumsajili Neymar ni kujiweka katika ulazima wa kutemana na wachezaji kadhaa ili kuchangisha pesa za kujinasia upya maarifa ya nyota huyu matata mzawa wa Brazil.

Akimtambulisha beki Junior Firpo kwa mashabiki wa Barcelona mwishoni mwa wiki jana, Rais Josep Maria Bartomeu alisema kwamba hawezi kabisa kufutilia mbali uwezekano wa kumsajili tena mchezaji mwingine katika muhula huu wa uhamisho.

Kipindi cha usajili wa wachezaji kwa mujibu wa kalenda ya soka ya Uhispania kinatarajiwa kutamatika rasmi mnamo Septemba 2.

Licha ya Bartomeu kusisitiza hivyo, Cardoner ameshikilia kwamba haiwezekani kabisa kwa kikosi hicho kujinasia maarifa ya Neymar licha ya panda-shuka tele kati yake na vinara wa PSG.

“Sioni dalili zozote zinazoashiria uwezekano wa Neymar kurejea uwanjani Camp Nou msimu huu. Tunafahamu kwamba hafurahii kabisa hali na maisha ya PSG. Pengine tumshawishi kwa mkopo. La sivyo, hiyo ni dili ambayo huenda ikarasimishwa msimu ujao,” akasema Cardoner.

Asalia nje

Neymar alisalia nje ya kikosi cha PSG kilichowakomoa Rennes 2-1 mwishoni mwa wiki jana na kutia kapuni ufalme wa Trophee des Champions jijini Shenzhen, China. Mabao ya PSG katika kivumbi hicho yalifumwa wavuni na Kylian Mbappe na Angel Di Maria.

Ingawa hivyo, Neymar aliyevutwa ugani na Marco Verratti mwishoni mwa mechi, alijumuika na wenzake kwa sherehe ya kutawazwa licha ya kuzozana peupe na Mbappe.

Neymar alirejea kushiriki mazoezi na PSG mnamo Alhamisi baada ya kusalia mkekani kwa kipindi kirefu tangu apate jeraha la kifundo cha mguu wakati wa mechi ya kirafiki iliyokutanisha Brazil na Qatar mnamo Juni. Jeraha hilo lilimweka nje ya fainali za Copa America.

Chini ya mkufunzi Thomas Tuchel, PSG watafungua kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) dhidi ya Nimes mnamo Jumapili.