Michezo

Barca yalishwa kichapo kocha Setien akijilaumu

January 27th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

VALENCIA, Uhispania

KOCHA Quique Setien amekiri huenda hakutoa maagizo mazuri baada ya vijana wake wa Barcelona kuaibishwa 2-0 na Valencia kwenye Ligi Kuu (La Liga), Jumamosi.

Mabingwa watetezi Barcelona, ambao walikuwa na mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora duniani Lionel Messi, walimiliki mpira uwanjani Mestalla lakini hawakupata mabao.

Valencia iliunda nafasi nyingi nzuri pamoja na kufunga mabao yalioifanya kuvuna alama zote tatu.

Kipa Marc-Andre Ter Stegen aliokoa Barca katika kipindi cha kwanza ikiwemo kupangua penalti ya Maximiliano Gomez dakika ya 12, baada ya Gerard Pique kuangusha Jose Gaya ndani ya kisanduku kabla ya kugusa shuti la Gomez na kulifanya ligonge mwamba.

Valencia haikuwa imepiga Barcelona uwanjani humu tangu Februari 2007.

Pia ilikuwa bila ushindi dhidi ya wapinzani hawa tangu Aprili 2016.

Lakini hapa ilipata bao la kwanza dakika tatu tu baada ya kipindi cha pili kuanza.

Jordi Alba alijifunga goli alipogusa shuti la Gomez, ambaye aliimarisha uongozi wa Valencia zikisalia dakika 13 mechi itamatike.

Kocha Setien, ambaye alikuwa akiongoza Barca katika mechi ya pili ligini baada ya kujaza nafasi ya Ernesto Valverde, alisikitishwa na jinsi vijana wake walicheza kipindi cha kwanza.

Alisema hawakuelewa maagizo yake, lakini akakiri huenda kosa lilikuwa lake. Katika mahojiano baada ya mechi Setien alisema: “Nadhani dakika 45 za kwanza tulicheza vibaya sana. Hatukujipanga katika nafasi zetu vyema, tulikosa shabaha. Walikuwa na nafasi tano ama sita. Lazima tutathmini vitu vingi kutoka kipindi cha kwanza.

“Kuna vitu ambavyo kabisa hatukushika; pengine sikutoa maelezo ya kufaa kwa wachezaji wangu.”

Ushindi wa Valencia ulidumisha rekodi yake ya kutoshindwa nyumbani msimu huu. Gomez anaamini Valencia ilistahili ushindi huo.

Alinukuliwa na tovuti ya klabu hiyo akisema, “Nafurahi sana kusaidia timu yangu; tulistahili ushindi huu. Sasa, hatufai kulegeza kamba.”

Barca iliingia mchuano huo ikishikilia nafasi ya kwanza kwa alama 43, mbele ya mahasimu wa tangu jadi Real Madrid kwa tofauti ya ubora wa magoli. Real iliratibiwa kumenyana na Valladolid jana usiku.

Katika matokeo mengine Jumamosi, Alaves ilichapwa 2-1 na Villarreal, Sevilla ikakanyaga Granada 2-0 nayo Espanyol ikatoka 1-1 dhidi ya Athletic Bilbao.