Michezo

Barca yawazia maisha bila Messi

February 11th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Barcelona imeanza kujiandaa kwa maisha bila supastaa Lionel Messi. Mshambuliaji huyu matata kutoka Argentina amekuwa mali ya Barcelona tangu mwaka 2001 akichezea timu ya makinda kwanza kabla ya kuingia ile ya watu wazima akiwa na umri wa miaka 17 mnamo Oktoba mwaka 2004.

Tangu wakati huo, ameifungia Barca zaidi ya mabao 500. Alianza kupata umaarufu mkubwa akiwa na umri wa miaka 20 baada ya Mbrazil Ronaldinho kuishiwa na makali mwaka 2007.

Ni katika mwaka huo pale alipobandikwa na vyombo vya habari vya Uhispania jina la utani Messiah. Uweledi wake wa kusakata soka ulimfanya kutawazwa mwanasoka bora duniani mwaka 2009, 2010, 2011, 2012 na 2015.

Amekuwa tegemeo wa Barca. Ameisaidia kushinda zaidi ya mataji 30 yakiwemo manne ya Klabu Bingwa Ulaya na tisa ya Ligi Kuu ya Uhispania.

Messi atagonga umri wa miaka 32 hapo Juni 24, 2019.

Sasa ripoti zinasema Barca imeanza kuona siku zake na mchezaji Messi zimeanza kuhesabika. Kwa mujibu wa gazeti la Express, rais wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu, anasema shughuli zao za kujisuka wakati huu zinachukulia kwa uzito kwamba siku moja Messi ataangika daluga zake.

“Najua siku moja Lionel atasema anastaafu,” Bartomeu aliambia Shirika la Utangazaji la BBC majuzi.

“Lazima tuandae klabu kwa siku za usoni. Tunaleta wachezaji wazuri walio na umri mdogo kikosini kwa sababu tunahitaji kuendeleza kipindi hiki cha mafanikio. Hilo ni jukumu letu.”

Baadhi ya makinda Barca imesajili majuzi ni mshambuliaji Mfaransa Masour Ousmane Dembele na kiungo Mbrazil Malcom Filipe Silva de Oliveira.