Michezo

Barcelona kuajiri Koeman kujaza nafasi ya kocha Setien

August 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BARCELONA wamemfuta kazi kocha Quique Setien siku tatu baada ya miamba hao wa Uhispania kudhalilishwa kwa kichapo cha 8-2 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Lisbon, Ureno.

Mkufunzi wa sasa wa timu ya taifa ya Uholanzi, Ronald Koeman aliyewahi kuvalia jezi za Barcelona kati ya 1989 na 1995 anatarajiwa sasa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Setien uwanjani Camp Nou.

Setien ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Real Betis, aliajiriwa na Barcelona mnamo Januari 2020 na alikuwa amesimamia jumla ya mechi 25 za Barcelona hadi kutimuliwa kwake.

Chini ya Setien, 61, Barcelona walikamilisha kampeni zao za msimu huu bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2013-14.

Barcelona walikamilisha msimu huu kwenye La Liga katika nafasi ya pili kwa alama tano nyuma ya mabingwa Real Madrid.

Kwa mujibu wa usimamizi wa Barcelona, kocha mpya atatambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki katika kipindi cha “siku chache zijazo”.

Mkufunzi wa sasa wa timu ya taifa ya Uholanzi, Ronald Koeman aliyewahi kuvalia jezi za Barcelona kati ya 1989 na 1995 anatarajiwa sasa kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Barcelona kumfuta kazi kocha Quique Setien. Picha/ AFP

Kichapo ambacho Barcelona walipokezwa na Bayern kwenye UEFA kilikuwa cha nne katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambayo iliwabandua kwenye robo-fainali za kipute hicho cha bara Ulaya.

Setien ambaye alimrithi kocha Ernesto Valverde uwanjani Camp Nou, amesema “huu umekuwa wakati mwafaka kwa usimamizi kuchukua maamuzi ya kuanza kukifanyia kikosi cha Barcelona mabadiliko muhimu kwa minajili ya kampeni za misimu ijayo.”

Baada ya kumtimua Setien, Barcelona walisema: “Haya ndiyo maamuzi ya kwanza kati ya mengi ambayo tunalenga kuchukua katika juhudi za kukisuka upya kikosi.