Michezo

Barcelona kukosa huduma za Gerard Pique kwa miezi minne ijayo

November 23rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique atakuwa nje kwa kipindi cha miezi mitatu na minne ijayo kutokana na jeraha baya la goti alilolipata wakati wa mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) dhidi ya Atletico Madrid waliowapiga 1-0 mnamo Novemba 21, 2020.

Mbali na Pique, 33, Barcelona watakosa pia huduma za Sergi Roberto ambaye pia atakosa kuwa sehemu ya mechi za Barcelona kwa miezi miwili ijayo kutokana na jeraha la paja.

“Madaktari wamefanya tathmini yao na kutuarifu kwamba Pique atalazimika kuwa nje kwa takriban miezi minne ijayo kuuguza jeraha baya la goti,” akasema kocha Ronald Koeman kwa kusisitiza kwamba tukio hilo ni pigo kubwa kwa safu ya ulinzi kambini mwa Barcelona.

Ushindi wa 1-0 ambao ulisajiliwa na Atletico dhidi ya Barcelona uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 20, moja nyuma ya viongozi Real Sociedad.

Kwa upande wao, Barcelona ambao walipoteza mchuano wao wa tatu kati ya mechi nane zilizopita walisalia katika nafasi ya 11 kwa alama 11 sawa na Valencia na Osasuna.