Michezo

Barcelona Ladies watazamiwa kutwaa ubingwa Chapa Dimba

April 21st, 2019 2 min read

NA JOHN KIMWERE

TIMU ya Barcelona Ladies inatazamiwa kuwa kati ya vikosi vya kuogopwa kwenye fainali za kitaifa kuwania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu. Kocha wake, Emman ‘Gullit’ Wambuchi amesema hayo kwa kuzingatia mwanzo kushiriki kipute hicho.

Barcelona Ladies ya Kaunti ya Laikipia ilisonga mbele ilipoibuka malkia katika Mkoa wa Kati kwa kuzoa mabao 2-1 dhidi ya bingwa mtetezi, Limuru Starlets katika fainali iliyopigiwa Thika Stadium, mjini humo.

Kwenye mechi hizo, Miriam Lutomia na Eunice Alele waliibuka mchezaji bora na mlinda lango bora mtawalia huku Jane Njeri akitwaa tuzo ya mfungaji bora.

Kwenye nusu fainali, Barcelona ilinyanyua Kirinyaga Dynamo kwa mabao 4-1 nayo Limuru Starlets ilisajili bao 1-0 mbele ya JYSA. ”Tuna furaha tele tulishusha mechi safi na kujikatia tiketi ya fainali pia nilifaulu kufunga magoli sita ndani ya mechi mbili,” Jane Njeri alisema.

”Tukwenda kukabili ushindani mkali lakini wapinzani wetu wakizubaa tu tutafanya makubwa,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa vigoli wake wamejiweka imara kuonyesha ujuzi wao katika ngarambe hiyo inayotazamiwa kushushudia msisimko wa kufa na kupona mwaka huu. Kadhalika alidokeza kwamba timu za Mkoa ya Nyanza na Rift Valley ndizo zitakuwa tisho kuu kwa kikosi chake.

Alisema wanalenga kuanza mazoezi kujinolea michuano hiyo itakayochezwa mwezi Juni mwaka huu, Uwanjani Kinoru Stadium Kaunti ya Meru.

Harriet Nasambu wa Barcelona Ladies (kulia) akijaribu kumpokonya mpira mpinzani wake Nancy Wanjiru wa Limuru Starlets kwenye fainali ya Chapa Dimba na Safaricom katika Mkoa wa Kati iliyopigiwa Uwanjani Thika Stadium, mjini humo. Barcelona ilishinda kwa mabao 2-1 na kufuzu. Picha/ John Kimwere

Kocha huyo anatoa mwito kwa Shirikisho la Soka la Kenya(FKF) pia Safaricom kuanzisha mpango wa kuwatambua makocha wanaonoa timu za mchezo huo mashinani.

”Hakika mtindo huo siyo sawa makocha pia wanastahili kutuzwa kwa mchango wao maana baadhi yetu huwa tumejitolea wala hatuna mshahara tunaolipwa,” alisema na kudai pia wanahitaji mafunzo zaidi kujiongezea maarifa.

Kadhalika alidokeza kuwa siyo vyema kwa kocha ambaye hunoa timu za wanaume kuteuliwa kufunza vikosi vya wasichana kulingana na uzoefu wake.

Alidai kocha wa wasichana anafahamu jinsi ya kuwafunza kwa kasi ya chini kinyume na wavulana.

Barcelona Ladies inajumuisha:

Harriet Nasambu 9nahodha), Eunicew Alele, Martha Nafula, Julia Liseina, Eunice Arivizia, Lavinda Jepchirchir, Marcella Nyabonyi, Miriam Lutomia, Jane Njeri, Naomi Masinde na Ruth Naserian. Pia wapo Faith Kaleche, Hellen Wangui, Phyllis Nduati, Dellness Nashipae na Cecilia Lesibia.

Kocha huyo pia anashukuru shabiki sugu wa kikosi hicho Christine Angeline aliyekuwa mstari wa mbele kuwapigia debe.

Kadhalika anatoa anashukuru wote waliwaochangia ufanisi wa kikosi hicho ikiwamo mwanzilishi wa Wakfu wa wasichana wa Samburu (SGF), Josephine Kulea, mwalimu mkuu Falling Waters Secondary school, Wachira Gitahi bila kusahau Elsie Wambura meneja wa timu hiyo.

Timu zingine ambazo tayari zimenasa tiketi ya fainali za kitaifa ni pamoja na St Marys Ndovea-wasichana (Eastern) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Western) pia Manyatta Boys na Ndhiwa Queens (Nyanza) bila kusahau wenzao Euronuts Boys (Kati).