Barcelona na Boca Juniors kupimana ubabe kwenye kipute kipya cha Maradona Cup

Barcelona na Boca Juniors kupimana ubabe kwenye kipute kipya cha Maradona Cup

Na MASHIRIKA

BARCELONA watamenyana na Boca Juniors katika mchuano wa mkondo mmoja wa kirafiki ili kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa jagina wa soka nchini Argentina na klabu ya Napoli, Diego Maradona.

Vikosi hivyo viwili vitakutana mnamo Disemba 14, 2021 katika uwanja wa Mrsool Park jijini Riyadh, Saudi Arabia kwa ajili ya kivumbi hicho cha Maradona Cup.

Maradona aliwahi kuchezea Boca kwa awamu mbili na alistaafu ulingoni akivalia jezi za kikosi hicho mnamo 1997. Aliwahi pia kuvalia jezi za Barcelona kwa kipindi cha misimu miwili kabla ya kujiunga na Napoli mnamo 1984.

Maradona aliyeongoza Argentina kunyanyua Kombe la Dunia mnamo 1986, aliaga dunia mnamo Novemba 2020 akiwa na umri wa miaka 60 baada ya kupata matatizo ya moyo.

Akiwa Boca, Maradona aliongoza kikosi hicho kutwaa taji la Metropolitano mnamo 1981 kabla ya kuyoyomea Barcelona alikoshinda mataji ya Copa del Rey, Copa de la Liga na Supercopa de Espana.

Alinyakua pia mataji mawili ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) akichezea Napoli na aliongoza Argentina kunyanyua kombe la pili la dunia miaka 35 iliyopita nchini Mexico.

You can share this post!

Zaidi ya vyuo 500 vya udereva hatarini kufungwa

Dybala aokoa Juventus kinywani mwa Inter Milan katika gozi...

T L