Barcelona na Sevilla watoshana nguvu kwenye La Liga

Barcelona na Sevilla watoshana nguvu kwenye La Liga

Na MASHIRIKA

BARCELONA walikamilisha kampeni zao za mwaka 2021 kwa matao ya chini baada ya kulazimishiwa sare na Sevilla waliokamilisha mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani.

Ushindi kwa Barcelona ya kocha Xavi Hernandez ungeshuhudia Barcelona wakipaa kwenye msimamo wa jedwali la La Liga hadi nafasi ya nne. Sevilla waliwekwa uongozini na Alejandro Gomez aliyekamilisha pasi maridadi kutoka kwa Ivan Rakitic katika dakika ya 32.

Ronald Araujo alisawazishia Barcelona mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Jules Kounde kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga Jordi Alba kwa mpira katika dakika ya 64. Kuondolewa kwa Kounde kuliwapa Barcelona fursa ya kushambulia zaidi ila wakapoteza nafasi nyingi za wazi kupitia Gavi na Ousmane Dembele.

Mvamizi Luuk de Jong alitokea benchi mwishoni mwa kipindi cha pili ila akashindwa kumzidi ujanja kipa Bono wa Sevilla. Barcelona kwa sasa wanakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 28, moja nyuma ya Real Sociedad na mabingwa watetezi Atletico Madrid wanaofunga orodha ya tano-bora.

Barcelona watavaana na Mallorca ugenini katika mchuano wao ujao wa Januari 2, 2022 kwa matarajio kwamba mwaka mpya utawaletea heri baada ya kuagana na supastaa Lionel Messi, kumfuta kazi kocha Ronald Koeman na kudenguliwa mapema kwenye hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwaka huu wa 2021.

You can share this post!

Real Madrid kusajili Joe Gomez wa Liverpool kuziba pengo la...

Spurs yakung’uta West Ham na kutinga nne-bora Carabao...

T L