Barcelona wakamilisha La Liga msimu huu kwa alama chache zaidi tangu 2008 baada ya kutandikwa na Villarreal

Barcelona wakamilisha La Liga msimu huu kwa alama chache zaidi tangu 2008 baada ya kutandikwa na Villarreal

Na MASHIRIKA

BARCELONA walitamatisha kampeni zao za msimu huu kwa kupoteza mechi yao ya nyumbani dhidi ya Villarreal na hivyo kukamilisha msimu kwa idadi ndogo zaidi ya alama chini ya miaka 14.

Villarreal waliotinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, walifuzu kwa soka ya Europa Conference League baada ya kupepeta Barcelona ugani Camp Nou.

Alfonso Pedraza alifungulia Villarreal ukurasa wa mabao kwa kujaza kimiani krosi ya Dani Parejo katika dakika ya 41 kabla ya Moi Gomez kufanya mambo kuwa 2-0 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya Adama Traore.

Bao la Frenkie de Jong wa Barcelona halikuhesabiwa na refa kwa madai kwamba alicheka na nyavu za wageni wao akiwa ameotea.

Barcelona waliambulia nafasi ya pili kwenye La Liga msimu kwa alama 73 huku pengo la pointi 13 likitamalaki kati yao na mabingwa Real Madrid.

Mara ya mwisho kwa Barcelona kujizolea idadi ndogo zaidi ya alama ligini ni 2007-08 walipokamilisha msimu kwa pointi 67.

Kwingineko, nambari nne Sevilla walishinda 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao waliokosa fursa ya kufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao. Atletico Madrid walikamilisha kampeni zao ligini katika nafasi ya tatu baada ya kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya nambari sita, Real Sociedad.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hofu Mswada kusukuma raia kwa bidhaa ghushi

AC Milan washinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada...

T L