Barcelona wampa Messi mkataba mpya wa miaka miwili

Barcelona wampa Messi mkataba mpya wa miaka miwili

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Manchester City na Paris Saint-Germain (PSG) kujitwalia huduma za nyota Lionel Messi yanazidi kudidimia baada ya rais wa Barcelona, Joan Laporta, kufichua kwamba sogora huyo raia wa Argentina anakaribia kurefusha mkataba wake ugani Camp Nou kwa miaka miwili zaidi.

Kandarasi ya sasa kati ya Barcelona na Messi, 33, inatamatika rasmi mwishoni mwa mwezi ujao.

“Tuna pendekezo ambalo tunatarajia Messi alikubali. Ahadi kubwa niliyotoa kwa mashabiki nilipokuwa nawania urais wa Barcelona ni kumshawishi Messi kusalia Camp Nou. Tutajitahidi kuhakikisha kwamba ahadi hiyo inatimizwa,” akasema Laporta, 58.

“Mambo yanakwenda vizuri na dalili zote zinaashiria kwamba atatia saini kandarasi mpya. Uhusiano wetu ni mzuri na Messi anaipenda sana Barcelona. Tungetamani astaafu soka akivalia jezi zetu japo ana uwezo wa kupata ofa nzuri zaidi kwingineko iwapo atateua kuondoka,” akaongeza kinara huyo.

Laporta aliyemrithi Josep Maria Bartomeu ndiye alifanikisha mpango wa Barcelona kuajiri Pep Guardiola ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Man-City. Guardiola aliwahi kuwa kocha wa Barcelona kati ya 2008 na 2012 chini ya Laporta aliyekuwa rais wa miamba hao kwa mara ya kwanza kati ya 2003 na 2010.

Messi aliwatumia Barcelona barua ya kutaka wamwachilie atafute hifadhi mpya kwingineko mnamo Agosti 2020. Hata hivyo, mpango wake wa kubanduka ugani Camp Nou ulitibuka baada ya kubainika kwamba kifungu kwenye mkataba wake na Barcelona kilihitaji kikosi chochote kinachomezea huduma zake kuweka mezani kima cha Sh87 bilioni.

Tangu Messi afichue azma ya kuagana na Barcelona, mshambuliaji na nahodha huyo amekuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Man-City kuungana na Guardiola huku akiwaniwa pia na PSG.

“Messi ana uamuzi wa ama kuondoka Barcelona au kusalia Camp Noun a kuwa sehemu ya mabadiliko yatakayofanywa na kikosi hicho kinacholenga kujisuka upya chini ya Laporta. Iwapo atafichua kwamba yuko kuondoka, basi tutamtwaa ili atusaidie kunyanyua taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akasema kocha wa PSG, Mauricio Pochettino anayemezewa upya na Tottenham Hotspur.

Messi alikosa mechi ya mwisho msimu huu dhidi ya Eibar baada ya waajiri wake kumpa likizo ya mapema ili aanze kujiandaa kwa fainali za Copa America zitakazofanyika Argentina kati ya Juni 13 na Julai 10.

Kati ya wanasoka wa haiba kubwa zaidi ambao wamefichua azma ya kuagana na Barcelona iwapo Messi atajiengua, ni mabeki raia wa Uhispania Gerard Pique na Jordi Alba.

Fowadi Sergio Aguero atakayevunja ndoa kati yake na Man-City mwishoni mwa msimu huu, yuko pua na mdomo kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona ambao pia wanavizia maarifa ya Eric Garcia (Man-City), Georginio Wijnaldum (Liverpool), Memphis Depay (Olympique Lyon) na Lisandro Martinez wa Ajax.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Barcelona pia wana mpango wa kubadilishana idadi kubwa ya wachezaji Inter Milan na Juventus kwa mkopo. Beki raia wa Uholanzi, Matthijs de Ligt ni miongoni mwa wachezaji ambao wanatarajiwa kuondoka Juventus na kutua Barcelona kwa mpango huo.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu katika nafasi ya tatu jedwalini nyuma ya Real Madrid na mabingwa Atletico Madrid. Ni mara ya kwanza kwa mabingwa hao mara 26 wa La Liga kukamilisha kampeni za kipute hicho nje ya mduara wa mbili-bora tangu 2007-08.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFYA: MKU yazindua kituo cha wahadhiri, wanafunzi kufanyia...

Majumba 2,000 ya kisasa kujengwa Gatanga na Juja